
Jeshi la Polisi limekwama
kuwafikisha mahakamani viongozi wanne wa Taifa wa Baraza la Vijana la Chadema
(Bavicha), baada ya kukosea hati ya mashtaka.
Wanaoshikiliwa ni Mwenyekiti wa
Taifa, Patrobas Katambi, Katibu Mkuu, Julius Mwita, Mjumbe wa Kamati ya
Utendaji, Joseph Kasambala na Mwenyekiti wa Mkoa wa Mbeya, George Tito.
Akizungumza jana, Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa alisema makosa yametokea wakati wa uandaaji wa
hati ya mashtaka.
“Mahojiano yameisha, charge
sheet (hati ya mashtaka) ikaandaliwa, lakini ikarudishwa tuifanyie marekebisho.
Muda umepita wa Mahakama watapelekwa kesho (leo),” alisema.
Hata hivyo, alisema kesi hiyo haina
dhamana kwa upande wa kituo cha polisi na hivyo kuwalazimu watuhumiwa hao
kuendelea kukaa rumande.
“Wasubiri kesho (leo) wataka-
poenda mahakamani kama wataamua kuwapa dhamana,” alisema
Mambosasa.
Kuhusu baadhi ya watuhumiwa hao
kugawanywa katika selo tofauti za Chamwino na wengine kuachwa Kituo Kikuu cha
Polisi, Mambosasa alisema huo ni utaratibu wa kawaida ambao unalenga kupata
maelezo ya kila mmoja.
“Hayo ni mahojiano tu ili kila
mmoja upate anasema nini ndipo unawaweka sehemu tofauti. Hizo ni taratibu za
mahojiano ili wasiendelee na mawasiliano,” alisema.
Makamu Mwenyekiti wa Bavicha,
Patrick Ole Sosopi alisema kisheria watuhumiwa hawatakiwi kukaa rumande kwa
zaidi ya saa 24.
“Cha kusikitisha siku ya leo (jana)
ambayo walisema wangewaleta mahakamani kwa kile wanachoamini wametenda kosa,
lakini hadi sasa muda wa mahakama unaisha viongozi wetu hawajaletwa,”alisema na
kuongeza:
“Na sisi tunataka kuondoka ili
tuone taratibu nyingine ambazo zinaweza kutuhakikishia usalama wa viongozi
wetu. Hadi sasa viongozi wetu hawajaletwa mahakamani.”
Alisema hata kama polisi wanawaona
viongozi wao wanamakosa, kisheria hawawezi kukaa na mtu kwa muda wa siku tatu
bila kumfikisha mahakamani.
Alisema utendaji wa polisi nchini
ni tofauti na wa nje ya nchi ambapo kwa nchi za wengine, polisi ni sehemu ya
huduma na si ya mabavu.
Alisema hali hiyo inaleta
kadhia na masumbuko kwa Watanzania na hivyo kupunguza imani yao kwa jeshi hilo.
Wakili wa watuhumiwa hao,
Fred Kalonga alisema wamekuwa na wateja wao tangu siku walipokamatwa kwa
kuhakikisha wanahojiwa kwa mujibu wa sheria.
“Kwa mujibu wa ahadi za
polisi kuwa leo (jana) wanaletwa mahakamani. Kuanzia saa 1.30 asubuhi tuko
mahakamani na sasa inakwenda saa 9.30 alasiri hakuna mtuhumiwa aliyeletwa.
Kimsingi muda wa mahakama umeisha,” alisema.
Alisema yeye na wakili mwenzake,
Azack Mwaipopo walikuwa wanakwenda kufuatilia taratibu nyingine za kisheria za
kuwawezesha kupata dhamana.
“Tunakwenda kufuatilia taratibu
nyingine lakini sisi tupo tayari muda wowote wakiletwa tutawadefend
(tutawatetea) kwasababu tunaamini kwa mujibu wa maelezo ya wateja wetu wapo
sahihi kuliko tuhuma zinazowakabili,” alisema.
Wanachama wa Chadema walikuwa
katika viwanja vya mahakama tangu saa 2.00 asubuhi hadi saa 9.30 alasiri baada
ya kuelezwa na wakili wa watuhumiwa kuwa viongozi wa Bavicha hawatapelekwa
mahakamani tena.
Viongozi hao walikamatwa Ijumaa
usiku katika baa ya Capetown walipokwenda kunywa na kula chakula. Wanadaiwa kwa
tuhuma za kukusudia kuikashfu Serikali.
Akizungumzia mpango wa vijana wa
Chadema kuzuia mkutano wa CCM utakaofanyika Julai 23 mjini hapa, Sosopi alisema
wanaiheshimu kauli ya Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe ya kuwataka
kutokwenda kuzuia mkutano huo.
“Tunaiheshimu kauli ya mwenyekiti
na tunatambua kuwa vijana wengi nchi nzima wamejiandaa kwenda kuzuia mkusanyiko
huo, lakini sasa tunashughulika na hili la viongozi wetu kukamatwa kwanza,”alisema.
Alisema baada ya viongozi wao
kupata dhamana wataitisha kikao cha Kamati ya Utendaji ya Bavicha haraka ili
kujadili suala hilo na watatoa msimamo kama wanakuja na mkakati mwingine ama
kuendelea na huohuo.

No comments:
Post a Comment