
ALIYEKUWA Spika wa Bunge la tisa,
Samuel Sitta, ameondolewa kwenye nyumba aliyokuwa akiishi baada ya Serikali
kugoma kumlipia kodi ya pango.
Kwa mujibu wa gazeti la Mtanzania, mwanasiasa huyo mashuhuri, aliondolewa katika nyumba hiyo iliyopo Masaki, Dar es Salaam na kulazimika kuanza kuhamisha vyombo vyake tangu Ijumaa ya Julai 8, mwaka huu.
Kwa muda wote tangu akiwa Spika wa
Bunge, Serikali ilikuwa inalipa kiasi cha dola 8,000 ambazo ni sawa na zaidi ya
Sh milioni 12 kwa ajili ya nyumba hiyo.
Sitta ambaye baadaye alikuwa waziri
katika Wizara ya Afrika Mashariki pamoja na Uchukuzi, aliendelea kuishi katika
nyumba hiyo kwa nafasi yake.
Kwa mujibu wa kijana aliyekuwa
nyumbani hapo, alisema walianza kuhama tangu mwishoni mwa wiki iliyopita na
wanaendelea kuhama kwa kuhamisha vitu kidogo kidogo.
“Ni kweli mzee amehama hapa, tangu
Ijumaa tulikuwa tunahamisha vyombo taratibu na sijui kama Serikali imegoma
kulipa kodi ama la, ila sasa amehamia jirani tu hapo Mtaa wa Manzese, hapa hapa
Masaki.
“Nasikia nyumba imepata mpangaji
mpya ndiyo maana wanahama,”alisema.
Alipotafutwa Mkuu wa Kitengo cha
Habari, Elimu na Mawasiliano wa Bunge, Owen Mwandumbya, ili kuzungumzia hilo,
alimtaka mwandishi kuwatafuta Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Wizara ya Fedha.
Alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa
utaratibu wa malipo kwa maspika wastaafu, ikiwa ni pamoja na matunzo na nyumba
wanazoishi, Owen alisema Bunge halihusiki na stahiki zozote za wastaafu kwa
mujibu wa sheria.
“Watafute Utumishi na Wizara ya
Fedha, wao ndio wahusika, Ofisi ya Bunge haihusiki na stahiki zozote za
wastaafu kwa mujibu wa sheria, isipokuwa Utumishi na Wizara ya Fedha ndio wahusika,” alisema.
Alipotafutwa Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki, alisema hana
taarifa hizo za kuondolewa kwa Sitta hivyo atafuatilia.
Hata hivyo, alipotafutwa tena
kupitia simu yake ya kiganjani, Kairuki alimtaka mwandishi kuwatafuta Hazina,
kwamba ndio wanaoweza kulisemea jambo hilo.
“Naomba uwatafute Hazina wakupe
ufafanuzi, halafu baadaye urudi kwangu,” alisema Kairuki.
Alipotafutwa Waziri wa Fedha na
Mipango, Dk. Philip Mpango kupitia simu yake ya kiganjani, ili kupata ufafanuzi
wa suala hilo, alisema:“Ufafanuzi kuhusu malipo kwa viongozi wastaafu
unatolewa kwa viongozi husika na si kwa vyombo vya habari.”
Hali hiyo ya Sitta, imekuwa ni
tofauti na aliyekuwa Spika wa Bunge la 10, Anne Makinda, ambaye Serikali
kupitia Bunge iligharimia matengenezo ya nyumba yake iliyoko Kijitonyama, Dar
es Salaam, ambako ujenzi wake ulikumbana na lawama kali za wananchi wanaoishi
jirani na eneo hilo.
Spika Makinda alilaumiwa na
majirani zake kwa kusababisha usumbufu baada ya kuziba njia inayopita katika
eneo hilo kwenda maeneo ya Sinza.
Kwa mujibu wa Margaret Sitta ambaye
ni mke wa Samweli Sitta na Mbunge wa Urambo, alisema kuwa walikuwa
wakiishi kwenye nyumba hiyo ya Serikali kwa kuwa mumewe alikuwa Waziri wa
Uchukuzi, lakini Baraza la Mawazili lilivunjwa tangu mwaka jana hivyo walipaswa
kuhama.
Chanzo: Mtanzania
Chanzo: Mtanzania

No comments:
Post a Comment