
Shirikisho la Vyama vya Tiba Asili
Tanzania (Shivyatiata) linakusudia kwenda mahakamani kufungua kesi dhidi ya Baraza
la Tiba za Asili likidai limewaadhibu kinyume cha sheria kwa kuwafungia
matabibu saba na vituo vya tiba hiyo.
Mwenyekiti wa Shivyatiata,
Abdulrahman Lutenga alisema jana kuwa Baraza hilo limewahukumu wenzao hao bila
kuzingatia vifungu vya sheria namba 23 ya tiba za asili na tiba mbadala ya
mwaka 2002, hivyo wameamua kwenda mahakamani kuomba tafsiri sahihi.
Lutenga alisema Shivyatiata
imepokea barua za malalamiko kutoka kwa waganga walioadhibiwa na Baraza hilo,
na baada ya kufanya uchunguzi wamebaini kwamba uamuzi huo ulitolewa bila
kuzingatia taratibu na sera na uendelezaji wa viwanda katika eneo la tiba
asili.
“Shivyatiata tunatambua kuwa Baraza
hilo ni chombo cha kitaalamu kwa mujibu wa Sheria namba 23 ya tiba za asili na
tiba mbadala hivyo lina mamlaka ya kuwaadhibu wanaokwenda kinyume cha sheria
hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa onyo au kumsimamisha mganga au mkunga na muuzaji
wa tiba za asili, lakini uamuzi uliochukuliwa na baraza hilo hatukubaliani
nao,” alisema Lutenga.
Alisema ingawa uamuzi unaweza
kutolewa bila kikao kwa kuwapelekea wajumbe nakala za shauri, mjumbe yeyote
anaweza kutaka uamuzi uahirishwe na suala hilo lijadiliwe katika kikao cha
Baraza, lakini cha kushangaza mwenyekiti wa Baraza hakukizingatia kifungu
hiki.
Alisema shirikisho hilo pia
linamuomba Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kutumia mamlaka aliyonayo kuwaondoa
watendaji wa Baraza hilo kwa madai kuwa wamekuwa wakiwadhalilisha na
kuwakatisha tamaa wanachama wake.
Katibu Mtendaji wa Shivyatiata
Othman Shem alisema wameshangazwa na uamuzi wa Baraza hilo kwa kuwa waganga
waliosimamishwa ni miongoni mwa waliokuwa wakiwategemea katika kuanzisha
viwanda vya tiba za asili kutokana na uwezo wa kifedha na kitaalamu
walionao.
“Baraza hili kweli linatakiwa
kuajiri watu ambao wanataaluma hii kwa sababu mazingira ya uamuzi yanaonyesha
umetolewa kwa lengo baya la kukandamiza taaluma yetu na kuturudisha nyuma kwa
hatua tulizoanza kupiga,” alisema.
Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili
na Tiba Mbadala, Dk Edmund Kayombo alitangaza uamuzi kukifutia usajili kituo
cha Foreplan kinachomilikiwa na Juma Mwaka kwa kutokidhi masharti ya usajili na
kufanya kazi kinyume cha usajili wake.

No comments:
Post a Comment