
Tanzania imeshauriwa kuongeza
vyanzo vipya vya mapato ya ndani kwa ajili ya maendeleo na kuchukua hatua kali
dhidi ya fedha haramu badala ya kutegemea mikopo ya nje.
Akizungumza jana jijini Dar es
Salaam katika utambulisho wa ripoti kuhusu Maendeleo ya Uchumi barani Afrika ya
mwaka 2016 ya Shirika la Maendeleo ya Biashara la Umoja wa Mataifa (UNCTAD),
Claudia Roethlisberger alisema mikopo siyo njia endelevu ya maendeleo.
Alisema licha ya ripoti hiyo
kuonyesha kuwa madeni ya nchi za Afrika yanahimilika, lakini Serikali za nchi
za bara hilo zinatakiwa kuchukua hatua ya kuzuia ukuaji wa haraka kwa madeni
ili yasiwe mgogoro kama ilivyotokea miaka ya mwishoni mwa 1980 na 1990.
Akizungumzia ripoti hiyo, mchumi
kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), Prosper Charle alisema mikopo yenye
masharti nafuu ambayo Tanzania imekuwa ikitegemea imepungua na kubaki yenye
masharti magumu, hivyo inapaswa kutafuta njia mbadala.
“Deni la Taifa kwa sasa
linahimilika kwa sababu Tanzania ilikuwa ikipata mikopo yenye masharti nafuu ,” alisema.
Steven Mwombela kutoka Taasisi ya
Utafiti wa Sera za kuondoa Umasikini (Repoa), alisema suluhisho kwa Tanzania ni
kuwekeza kwenye ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi ili kupata maendeleo
endelevu.

No comments:
Post a Comment