
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema
Serikali itahakikisha viwanda vinajengwa kwa wingi nchini kwani ndiyo msingi
imara wa ukuaji wa uchumi na muarobaini wa tatizo la ajira hususan kwa vijana.
“Mbali na kukuza uchumi na kuongeza
fursa za ajira nchini, viwanda hivi ndivyo vitakavyotufanya tununue bidhaa kwa
bei nafuu tofauti na ilivyo sasa kwa kuwa vitu vingi vinaagizwa kutoka nje ya
nchi,” alisema.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana
(Jumatano Julai 13, 2016) wakati akikagua ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza
vigae (Tiles) cha Goodwill Tanzania Ceramic katika kijiji cha Mkiu wilayani
Mkuranga, Pwani.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji
wa kiwanda hicho Bw. Frank Yang alisema jumla ya ajira 4,500 zinatarajiwa
kutolewa kiwandani hapo mara ujenzi utakapokamilika.
Akifafanua kuhusu ajira hizo Bw.
Yang alisema ajira 1,500 zitakuwa rasmi na zisizo rasmi zitakuwa 3,000 huku
wakazi wanaoishi katika maeneo yanayozunguka kiwanda hicho wanatarajiwa kupewa
kipaumbele. Mkurugenzi huyo alisema ujenzi wa kiwanda hicho utagharimu dola
milioni 100 na utafanyika kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza inatarajiwa
kukamilika Desemba mwaka huu.
“Ujenzi wa kiwanda hiki utainua
ukuaji wa uchumi nchini Tanzania kwani utakapokamilika Serikali itakusanya sh.
bilioni 30 kwa mwaka ikiwa ni mapato ya kodi,” alisema.
Naye Balozi wa China nchini
Tanzania Dk.Lu Youqing aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuchagua sekta ya
viwanda kuwa ndiyo kipaumbele chake katika kukuza uchumi. Alisema mbali ya
ujenzi wa kiwanda cha vigae katika eneo hilo pia wawekezaji hao kutoka nchini
China wanatarajia kujenga viwanda vya mbolea, karatasi na glasi (bilauli).
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
alipokea msaada wa madawati 500 yenye thamani ya sh milioni 40 ambayo
yalitolewa na Balozi wa China nchini Dk. Lu kwa kushirikiano na Mkurugenzi
Mtendaji wa Kiwanda cha Goodwill Tanzania Ceramic Bw. Yang.

No comments:
Post a Comment