
Zimebaki wiki tatu kabla Shirika la
Nyumba la Taifa (NHC) kuchukua jengo la Bilicanas lililokodiwa na Mwenyekiti wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, kuendesha biashara
ya ukumbi wa starehe.
Jengo hilo lipo eneo la Posta
jijini Dar es Salaam.Awali, NHC ilikuwa imetoa notisi ya siku 60 kwa wadaiwa
sugu ambao wamepanga katika majengo yake akiwamo Mbowe.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu, alisema pamoja na Bilicanas,
shirika linazidai taasisi za umma, binafsi na watu binafsi jumla ya Sh. bilioni
15.
Notisi ya siku 60 ya kuondoka
Bilicanas pamoja na majengo ya wadaiwa wengine ilishatolewa, Mchechu alisema na
kwamba sasa zimesalia wiki tatu.
Alisema baada ya muda huo
kumalizika, utekelezaji wa kuondolewa katika majengo hayo utaanza ukiambatana
na uchukuaji wa hatua za kisheria.
Mchechu alisema mbali ya Bilicanas,
wadaiwa wengine ni Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi inayodaiwa Sh. bilioni
mbili, Benki ya Azania (Sh. milioni 161) na Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano
wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa (Sh. milioni 631).
Wadaiwa wengine walitajwa kuwa ni
Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Sh. bilioni
1.3), Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sh. bilioni mbili), Tume ya
Utumishi (Sh. milioni 109) na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Sh.
bilioni moja.
Mchechu alisema ukusanyaji wa
madeni hayo kwa nguvu ni mkakati wa shirika hilo kukusanya fedha ili kusaidia
ujenzi wa nyumba za watumishi wanaohamia Dodoma.
Alipoulizwa iwapo mkakati huo una
uhusiano wowote na masuala ya kisiasa kutokana na kumtaja Mbowe kuwa ni kati ya
wadaiwa sugu, Mchechu alisisitiza hakuna uhusiano wa siasa na zoezi hilo kwani
wateja wote wanachukuliwa sawa.
“Mwaka huu ujenzi unaanza
Dodoma," alisema Mchechu, hivyo fedha tunazodai zitatusaidia kukamilisha
uwekezaji mjini humo."
“Ndiyo maana tumetoa kwa tunaowadai
notisi ya miezi miwili, vinginevyo wataondolewa katika majengo ya shirika kama
kanuni zinavyotaka.
“Hakuna uhusiano wowote kati ya
shirika kukusanya fedha linazodai na watu binafsi akiwamo Mbowe, taasisi za
umma na binafsi.
“Lengo ni kukusanya madeni ambayo
baadhi yake yalisimama kutokana na mengine kuwa na kesi mahakamani.”
Alisema kuwa fedha hizo zitatumika
kwa ujenzi wa nyumba za watumishi 300 hadi 500 mkoani Dodoma.
Alisema ujenzi huo unatarajia
kuanza mara moja na utachukua miezi 12.
Kwa mujibu wa Mchechu, Sh. bilioni
60 za ujenzi wa nyumba hizo zitatokana na fedha za ndani.
Alisema shirika hilo limenunua
ekari 240 eneo la Iyumbu, ekari saba Chamwino, nne Bahi na Chemba ekari nne pia
ikiwa ni kuunga mkono azma ya Serikali ya Awamu ya Tano kuhamia Dodoma.
Alisema fedha nyingine zitapatikana
baada ya nyumba 97 za shirika hilo zilizopo Medeli mjini Dodoma kuuzwa.
Aidha, Mchechu alisema kitendo cha
Serikali kuhamia Dodoma kitatoa fursa kwa Jiji la Dar es Salaam kujiimarisha
kibiashara tofauti na ilivyo sasa ambapo linakwamishwa na foleni kubwa za
magari kutokana na shughuli nyingi za serikali kufanyika.
“Dar es Salaam kuna bandari, uwanja
wa ndege," alisema na kuongeza: “Hivyo suala la kiuchumi litaimarika zaidi
kutokana na shughuli nyingi za Serikali kuhamia Dodoma. Hii itasaidia uchumi wa
nchi kusambaa katika maeneo tofauti nchini.”
Uwekezaji wa NHC jijini Dar es
Salaam upo kwa asilimia 70, alisema na kwamba ufanisi wa Jiji utaongezeka
hususani katika usafiri na sekta nyingine kiuchumi.

No comments:
Post a Comment