Habari mheshimiwa
waziri, nina imani ni mzima wa afya, pole na hongera kwa kazi ngumu unayofanya
kwa moyo mmoja katika wizara yako. Mimi ni kati ya wananchi tuliojiajiri katika
tasnia ya filamu hapa nchini, japo hali ni mbaya mno lakini tunaendelea
kujikongoja hivyo hivyo tukisubiri uharamia ukomeshwe kwa asilimia kubwa ili
tupumue kidogo kama watu wa shuguli zingine za kiuchumi.
Mheshimiwa kisa cha kushika hii kalamu ni baada ya
kusoma habari za kukamatwa kwa vijana wa Orijino Komedi hapo majuzi kwa kosa la
kuvaa sare za jeshi la polisi kitendo ambacho ni kinyume na sheria za nchi
yetu. Lengo ni kuzungumzia hilo suala ila kwakuwa hii nafasi ya kuongea na wewe
ni adimu, acha nitaongeza na mengine kidogo nje ya suala la sare.
Mheshimiwa mlivyosema kurasimisha tasnia ya filamu nina
imani mlimaanisha kwa ujumla wake, lakini kuna kipindi nashawishika kuwa maana
ya kurasimisha iliishia kwenye kuweka stika za TRA kwenye kava za DVD basi.
Maana mi ninaamini kama tasnia ingerasimishwa katika ujumla wake na
ikafuatiliwa haswa, mpaka muda huu tungekuwa pazuri maana muda umepita kidogo
mheshimiwa
Kwa suala la sare mheshimiwa ni kitu kidogo mno ambacho
kama kweli kuna urasimishaji, kusingekuwa na tatizo kama la Orijino Komedi sasa
hivi. Najua kuna wazo linaweza kuja kuwa wale mabwana wamevaa kwenye harusi
kwahiyo wana makosa na hoja yangu kuwa sio ya msingi hapa. Orijino Komedi
wanajulikana kazi yao na pale walikuwepo kazini bila kujali walilipwa au
walimfanyia free mwenzao.
Ile ni kazi ya sanaa, ila cha muhimu wamefanya kitu
ambacho wamezua mjadala na labda tuombe Mungu ndio uwe mwanzo wa kujadili kati
ya wadau wa filamu na serikali kuhusu mambo hayo ambayo ndio mjumuiko sahihi wa
maana ya urasimishaji.
Nilisema sare ni jambo rahisi kwa sababu tunataka hadi
silaha zenyewe, sio sare tu. katika filamu kuna kutumia bunduki zenyewe au za
bandia zinazofanana na za halisi(pellets guns), mheshimiwa tunahitaji vituo
halisi vya polisi kabla hatujaanza kujenga spesho kwa ajili ya filamu, tunabezwa
filamu zetu hazina uhalisia kwakuwa selo zetu watazamaji wetu wanajua kabisa
sio selo bali ni dukani kwa Mangi!
Mheshimiwa majiji kama New York, idara ya polisi (New
York Police Department /NYPD) wana kitengo kipo maalum kwa ajili ya kutoa
msaada kwa filamu, iwe sare, silaha, vituo vya polisi, mahakama, helikopta na
hata polisi wenyewe ikitakiwa watumike na vingine vingi na kuweka polisi kadhaa
katika location kufuatilia.
Mheshimiwa, New York, Los Angeles na majiji mengine huko
Marekani na Ulaya nimeenda mbali, hapa jirani yetu Afrika ya Kusini hata
ukikitaka kituo cha polisi wanakutajia bei ukilipa wanahamia uani mheshimiwa.
Siongei mambo ya kijiweni.
Nina uhakika na
ninachoongea, kumbukumbu zangu za mwisho ilikuwa 2011 Afrika Kusini ukitaka
helikopta ya polisi ilikuwa milioni mbili kwa saa, kumkodi polisi mmoja na sare
zake ilikuwa shilingi 130,000 kwa saa. Gari la polisi ilikuwa laki mbili kasoro
kidogo kwa saa. Ila pia unaweza kuomba kibali ukaweka helikopta yeyote stika ya
polisi, au hata magari.
Mheshimiwa,
serikali ya Afrika Kusini inatoa ushirikiano wa ajabu katika filamu, cha
kushangaza zaidi wizara ya viwanda na biashara wana kitengo cha kukopesha hela
kwa wazalishaji ili watengeneze filamu.
Mheshimiwa waziri, serikali ya Ufilipino ikimkuta mtu na
kosa la kuvaa sare za polisi (Philippines National Police /PNP) inamfunga jela
miaka minne na miezi miwili, lakini waigizaji wameruhusiwa kuvaa sare hizo
katika kazi zao. Mgogoro umetokea hapo majuzi baada ya muigizaji kuigiza
akisaula sare hizo katika muziki mbele za watu, ndani ya tamthilia iitwayo ‘On
the Wings of Love.’ Kwahiyo mheshimiwa, waigizaji waruhusiwe ila kwa masharti
maalum kama walivyofanya PNP Ufilipino.
Mheshimiwa, sisemi kila muigizaji au kampuni ya
uzalishaji iwe na sare au silaha la hasha, iwepo kampuni itakayoaminiwa na
serikali au kitengo katika wizara yako ambacho kitakuwa na mamlaka ya kumiliki
silaha, sare za polisi trafiki na kadhalika ambapo wazalishaji watakuwa
wanaenda kukodi kwa gharama nafuu na pia kinasimamia maeneo ambayo vifaa hivyo
vinatumika. Vitu hivyo vinaonekana ni vitu vidogo lakini ukweli hufanya filamu
ziwe na msisimko wa kipekee.
Mheshimiwa waziri, serikali ikisema kurasimisha tasnia ya
filamu isimaanishe kukusanya kodi tu peke yake, bali dhamira kuu iwe kuinua
filamu na kodi itapatikana, maAna hata hizo stika za TRA imekuwa ni tisha toto
tu maana wezi wapo wengi na wanajua stika zimewekwa kwa mikwara hakuna
anayezifuatilia. Tangu tasnia irasimishwe filamu ndio hamna biashara kabisaaa
afadhali hata kabla.
Kazi ya kufanya filamu ziuzike na wahusika tunufaike na
serikali ipate kodi yake ni kazi ndogo mno, ilimradi serikali iamue tu
mheshimiwa. Naomba wizara yako iamue sasa ili tunufaike na uwezo wetu tuliopewa
na mwenyezi Mungu.
Nawapa pole Orijino Komedi kwa matatizo yaliyowakuta,
lakini nashukuru pia maana imekuwa ni njia moja wapo ya kulizungumzia na kulipa
umakini jambo hili, kama kifo cha Kanumba kilivyotuumiza lakini ikawa ni njia
iliyofanya serikali istuke na igundue nguvu ya sanaa katika jamii.
Mheshimiwa naomba uwasaidie vijana wa Orijino Komedi
wasamehewe na uliweke sawa jambo hili, tunataka sare, silaha, vituo vya polisi,
mahakama, kufunga mitaa wakati tunashuti barabarani na mambo mengine
mengi.Mheshimiwa kuigiza vizuri hakupeleki sanaa ya filamu kokote kama hakuna
vitu vya uhalisia ndani ya filamu hizo.
Nashukuru kwa kutumia muda wako kusoma waraka huu
mheshimiwa waziri, kwa uchapakazi wako nina imani tasnia yetu ya filamu itafika
mbali kwa wakati huu ambapo ipo katika mikono yako. Asante.
Paul Sekaboyi 0753 666 444

No comments:
Post a Comment