
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewaagiza Wakuu wa Wilaya na Maofisa Elimu nchini wafanye ukaguzi katika shule
ili kubaini wanafunzi hewa kwenye mpango wa elimu bure.
“Kila mwezi Serikali inapeleka
shule zaidi ya shilingi bilioni 18 kugharamia elimu bure na sasa tumeanza kuona
udanganyifu katika sekta ya elimu kwa kuwa na wanafunzi hewa. Wakuu wa Wilaya
na Maofisa Elimu nendeni mkafanye ukaguzi ili mpate takwimu sahihi,“amesisitiza.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana
(Alhamisi, Agosti 18, 2016) alipokutana na watumishi na viongozi wa Manispaa ya
Ilala katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Nyerere jijini Dar es
Salaam.
“Wakuu wa Wilaya na Maofisa
Elimu mkiona takwimu ziwachanganya, ni lazima mtoke maofisini na kwenda katika
shule zilizo kwenye mpango wa elimu bure mkafanye uhakiki wa idadi ya
wanafunzi,” alionya.
Wakati huo huo Waziri Mkuu
amesema maamuzi yanayotolewa kwenye vikao vya madiwani lazima yawe na
tija na ameitaka halmashauri hiyo kuhakikisha fedha zinazokusanywa zinatumika
kuboresha shunghuli za maendeleo badala ya kujilipa posho.
“Lazima mjipange vizuri na kupunguza
changamoto zinazoikabili wilaya yenu. Malipo yote ni lazima yawe yale
yaliyoainishwa katika waraka na si vinginevyo.Mtu wa Ilala unadai nauli ya sh.
200,000; hivi unakuwa unatoka wapi hata mimi wa Lindi silipwi nauli hiyo,” alihoji.
Waziri Mkuu alisema ni lazima
halmashauri zote nchini zizingatie sheria za Mamlaka ya Serikali za Mitaa na
watendaji wake wajiulize kama mambo wanayoyafanya yana tija na wanawatendea
haki watu wanaowatumikia.
Alisema Serikali inataka kuwa na
watumishi wanaotambua nafasi zao na watakaofanya kazi kwa uadilifu, uaminifu
pamoja na uwajibikaji mkubwa hivyo kila mtu ahakikishe anafanya kazi vizuri na
yenye matokeo chanya.
“Kuna watu wanaona ukuu wa idara
ndiyo kila kitu, hata yule anayekimbiza mafaili hathaminiwi, hili si jambo
jema! Ninyi wote ni kitu kimoja, ni watumishi wa Serikali, hivyo kila mmoja
amthamini mwenzake,” alisema.
Waziri Mkuu alisema: “Mkurugenzi
yeyote asikubali kuwa na wakuu wa Idara wasiokuwa na ushirikiano na watumishi
wengine kwa sababu hataweza kupata mafanikio ya kiutendaji ndani ya eneo
lake,”.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM.
ALHAMISI, AGOSTI 18, 2016.

No comments:
Post a Comment