
BARAZA la Vijana la Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Bavicha), limetangaza kuunga mkono operesheni ya Umoja
wa Kupambana na Udikteta (Ukuta) iliyotangazwa hivi karibuni na Kamati Kuu ya
chama hicho.
Aidha, Bavicha wamemjibu Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kwamba hana mamlaka ya kuzuia operesheni
hiyo kwa kuwa wanaifanya kisheria na yeye siyo msajili wa vyama vya siasa.
Makonda aliagiza Jeshi la Polisi
kuzuia maandamano ya Ukuta, Ijumaa wakati akizungumza na Kikosi cha Kutuliza
Ghasia (FFU) katika kambi ya Ukonga.
Akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Bavicha, Patrobas Katambi, alisema
maandalizi ya kuunga mkono operesheni hiyo yamekamilika kwa nchi nzima.
“Kauli ya Mkuu wa Mkoa (wa Dar es
Salaam) ya kusema kwamba polisi wahakikishe Ukuta haujengeki, haitekelezeki kwa
sababu yeye hana mamlaka ya kufanya hivyo na wala si msajili wa vyama vya siasa
hadi atoe kauli hiyo,” alisema Katambi.
“Zipo kesi nyingi zinazoonyesha
wakuu wa mikoa kufanya kazi ambazo haziwahusu, hivyo kauli yake tutaipima
kisheria,” alisema na kuongeza:
“Yeye akitaka aendelee kusema
chochote akijisikia, lakini sisi tunamwambia kwamba mikutano yetu iko pale pale
na tutaifanya nchi nzima.”
Katika mazungumzo yake na FFU,
Makonda alisema askari wanafahamu sheria, hivyo wasisubiri mtu yeyote kuja
kuwakumbusha juu ya jambo hilo.
Aidha, aliwataka polisi hao
kutosubiri maelekezo mengine kwa kuwa Amiri Jeshi Mkuu ambaye ni Rais John
Magufuli ameshaagiza kutofanyika kwa maandamano ya Ukuta yaliyopangwa kuwa
Septemba mosi.
Makonda aliliagiza jeshi hilo
kuhakikisha kwamba sheria zinafuatwa na kusiwapo kitu kinaitwa Ukuta ili
wananchi waendelee na kazi zao kama kawaida.
Lakini Mwenyekiti wa Bavicha jana
alisema: “Tunamtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu,
ajiandae kutuma jeshi lake kulinda mikutano yetu.”
Kuhusu onyo la Rais Magufuli aliloitoa
akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Singida kwamba Chadema isimjaribu kwa
Ukuta, Katambi alisema chama hicho hakimjaribu.
Alisema Chadema itafanya maandamano
nchi nzima kwa sababu kwa njia hiyo wanamsaidia kutoa mawazo yao kama vyama vya
siasa kwa ajili ya kumsaidia kuendesha shughuli zake vizuri zaidi.
“Hatuna shida ya kumjaribu Rais, na
wala si kwamba tunamchukia, na wala hatuna sababu ya kupinga uwapo wake, na
hata ukiulizwa sasa kwamba Rais wako ni nani, lazima useme ni John Magufuli,” alisema
Katambi.
“Tunapotoa dosari na kasoro
tunamsaidia kuendesha nchi yake na watu walio chini yake.”
“Sisi kama vyama vya siasa tuna
haki, tunajua yeye ndiye Rais, kama sisi hatukuweza kupata nafasi ya hiyo,
haimaanishi kwamba ni vita, isipokuwa kupitia vyama vyetu, tuna sehemu ya kutoa
mawazo yetu katika kuifanikishia serikali yake kuongoza vema pamoja na watu
wake wa chini tena kwa mujibu wa sheria na inamsaidia yeye kuwa bora zaidi.
“Kwa hiyo kauli ya Rais sisi hatuna
tatizo nayo.”
Katambi alisema taratibu zote za
kisheria katika kutekeleza mikutano hiyo zitafuatwa.
Kamati Kuu ya chama hicho ilisema
lengo la operesheni hiyo ni kuzuia matukio ya ukandamizaji wa haki na
demokrasia nchini.

No comments:
Post a Comment