
Serikali ya Brazil imeonesha nia kuwekeza katika sekta ya nishati nchini hususan katika kuzalisha umeme kwa kutumia maji na mabaki ya miwa. Hayo yameelezwa jana jijini Dar es Salaam na Balozi wa Brazil nchini Tanzania, Carlos Alfonso Puente, alipomtembelea Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ofisini kwake na kufanya mazungumzo naye.
Balozi Puente alimweleza Profesa
Muhongo kuwa nchi yake inao ujuzi na uzoefu wa kutosha katika uzalishaji wa
umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali hususan maji.
Alisema, Brazil ingependa kuchangia
kufanikisha azma ya Rais John Magufuli kuifanya Tanzania kuwa nchi ya Viwanda.
“Kutekeleza mchakato wa kuifanya nchi kuwa ya Viwanda, unahitaji
umeme mwingi unaotokana na vyanzo mbalimbali. Ni bahati nzuri kwamba Tanzania
inazo njia za kufanikisha azma hiyo,” alisema.
Alisema kuwa, nchini Brazil, kuna
Kampuni kubwa zenye uzoefu wa muda mrefu unaofikia miaka 20 hadi 40 katika kazi
hiyo, ambazo huzalisha umeme wa maji nchini mwao na hata nje ya nchi.
Pia, alitaja eneo jingine ambalo
nchi yake ina nia ya kuwekeza kuwa ni uzalishaji wa umeme unaotumia mabaki ya
miwa ambayo aliielezea kuwa chanzo kizuri cha nishati safi.
Balozi Puente alisisitiza kuwa,
Brazil ikiwa ni nchi inayozalisha miwa kwa kiwango kikubwa duniani, itasaidia
kuleta mabadiliko katika sekta ya nishati kwa kuzalisha umeme unaotokana na
mabaki ya miwa kwa kutumia teknolojia za kisasa.
Kwa upande wake, Waziri Muhongo,
akimjibu Balozi Puente, alikiri kuwa kuwa Brazil ina ujuzi, uzoefu na uwezo
mkubwa hususan katika maeneo ambayo Balozi aliyataja na hivyo akamwambia nchi
hiyo inakaribishwa kuwekeza Tanzania kwa kufuata masharti na utaratibu
uliowekwa na Serikali.
Akizungumzia zaidi kuhusu utaratibu
wa uwekezaji, Waziri Muhongo alieleza kwamba Serikali ya Tanzania, kupitia
Wizara yake, inabadilisha utaratibu wa kupokea wawekezaji katika sekta husika.
Alisema, kunaandaliwa utaratibu
maalum utakaokuwa wa wazi na kuruhusu ushindani kwa wenye nia ya kuwekeza kwa
malengo ya kupunguza au kuondoa kabisa mazingira ya rushwa na muda mrefu
unaotumika katika majadiliano pasipo sababu za msingi.
Profesa Muhongo alifafanua zaidi
kwamba, Serikali itaweka mazingira mazuri zaidi ya ushindani kwa kuandaa
maelezo ambayo pamoja na mambo mengine yatabainisha aina mbalimbali za vyanzo
vya umeme vilivyopo nchini pamoja na maeneo vilipo.
Alisema, Kampuni zenye nia ya kuwekeza
zitakaribishwa kupendekeza viwango vya bei vitakavyotumika kuuza umeme
utakaozalishwa na zitashindanishwa, ambapo washindi wachache watachaguliwa kwa
ajili ya majadiliano kabla ya kuingia mkataba wa uwekezaji husika.
“Kwa hivyo, tunaandaa kabrasha maalum litakalokuwa na maelezo
husika na litakuwa tayari mwezi wa Septemba mwaka huu. Kabrasha hilo lenye
maelezo litatumika kama mwongozo wa ushindanishaji maombi mbalimbali ya
uwekezaji hususan katika kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali kwa uwazi,”
alisisitiza.
Alivitaja vyanzo hivyo kuwa ni
pamoja na gesi asilia, makaa ya mawe, maji, jua, upepo, jotoardhi, mawimbi ya
bahari pamoja na nishati mbadala. Waziri Muhongo alisema kuwa maelezo hayo
maalum yatasambazwa kwa wadau mbalimbali wa sekta husika wakiwemo wale wote
wenye nia ya kuwekeza ikiwa ni pamoja nan chi ya Brazil kupitia Ubalozi wake
hapa nchini.
“Kwa kutumia Kabrasha hilo maalum lenye maelezo husika, wewe
Balozi utaweza kuwashawishi wafanyabiashara kutoka nchini kwako kutoa
mapendekezo ya uwekezaji ambayo yana vigezo vyote muhimu vinavyoshawishi wapate
fursa husika za uwekezaji katika sekta ya nishati,” Profesa Muhongo alimweleza
Balozi Puente.
Kuhusu Mradi mkubwa wa ujenzi wa
Bomba la kusafirisha mafuta kutoka Uganda hadi Tanzania, ambao pia Brazil
imeonesha nia kuwa ingependa kuwekeza kwa kushirikiana na Tanzania; Profesa
Muhongo alisema Serikali itaweza kulisemea hilo baada ya kipindi cha miezi
takribani 45 kupita, ambapo mambo yote ya kisheria kuhusu Mradi huo
yanatarajiwa kuwa yamekamilika.
Aidha, Profesa Muhongo alitumia
fursa hiyo kuomba nafasi za masomo nchini Brazil kwa wanafunzi wa kitanzania
katika ngazi za Shahada za Uzamili na Uzamivu katika sekta ya Nishati hususan
Mafuta na Gesi, kwa kuzingatia kuwa Brazil imeendelea sana katika sekta hiyo.
“Ninyi mnazo Taasisi bora kabisa za Utafiti duniani. Mnafanya
vizuri sana katika maeneo mbalimbali.”
Kwa mujibu wa Profesa Muhongo,
Brazil ni miongoni mwa nchi Tano (5) bora duniani zinazozalisha umeme kwa
kutumia nishati jadidifu kwa sababu umeme mwingi wanaozalisha unatokana na
maji, kutoka katika Mito mikubwa waliyonayo.
Balozi wa Brazil nchini Tanzania, Carlos Alfonso
Puente (Kushoto), akisaini Kitabu cha Wageni ofisini kwa Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo (Kulia), alipomtembelea Waziri na kufanya naye
mazungumzo kuhusu ushirikiano baina ya nchi hizo mbili hususan katika uwekezaji
kwenye sekta ya nishati.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (Kushoto),
akimsikiliza kwa makini Balozi wa Brazil nchini Tanzania, Carlos Alfonso Puente
(kulia), wakati Balozi huyo alipomtembelea Waziri Ofisini kwake jijini Dar es
Salaam hivi karibuni na kufanya mazungumzo naye kuhusu masuala ya uwekezaji
katika sekta za nishati na madini. Wengine pichani ni Maafisa wa Wizara
waliohudhuria mkutano huo.

No comments:
Post a Comment