MFANYABIASHARA maarufu, Mustapha
Jaffer Sabodo ametangaza kutoa dola za Marekani bilioni 5 (Sh trilioni 10) kwa
ajili ya kuwekeza mkoani Dodoma, ikiwa ni njia ya kumuunga mkono Rais John
Magufuli kuhamisha makao makuu ya serikali kwenda mkoani humo.
Akizungumza Dar es Salaam jana,
Sabodo alisema atawekeza kiasi hicho cha fedha, iwapo serikali yote itahamia
mkoani humo, itakuwa ametimiza ndoto ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere
ambaye alitamani kuona mkoa huo unakuwa makao makuu ya nchi.
Alisema alichofanya Rais Magufuli,
kimewashinda marais wengine waliomtangulia, hivyo yeye kama mfanyabiashara na
mtu mwenye mapenzi makubwa kwa nchi yake, lazima aunge mkono hatua hiyo ya
Serikali kuhamia Dodoma ambayo aliita ‘Azimio la Dodoma’.
“Niliposikia anatangaza kwenye
televisheni ya taifa kwamba Serikali itahamia Dodoma, ilikuwa mara yangu ya
kwanza baada ya miaka mingi kupita, nilitabasamu moyoni, jambo ambalo
lilinitokea miaka 10 ya kwanza ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere.
“Leo nimesikia kutoka kwako nimeona
ile roho ya Nyerere imezaliwa tena.
“Kwa hiyo natangaza kuunga mkono
Azimo la Dodoma kwa kuwekeza dola za Marekani bilioni 5, ambazo zitatumika kwa
ajili ya uwekezaji mkubwa katika huduma mbalimbali za jamii mkoani humo,” alisema Sabodo.
Sabodo alisema atatoa fedha hizo
ili zitumike kuwekeza kwenye viwanda kama vya mvinyo, viwanda vya kusindika
mihogo na viwanda vingine ambavyo vitahitajika katika mkoa huo.
Alisema kuwepo kwa huduma hizo
mkoani Dodoma, kutasaidia kuufanya mji huo kukidhi matakwa ya watumishi wa umma
watakaohamia huko.
Mfanyabiashara huyo aliongeza kuwa
atafanya uwekezaji mkubwa huo kwa sababu lengo lake ni kuona mji wa Dodoma,
unaungana na miji ya jirani kama Mpwapwa, Kondoa na Manyoni ili kutoa fursa ya
kupanua huduma mbalimbali katika makao makuu hayo ya nchi.
Sabodo alisema kwamba juhudi zake
za kuwekeza katika huduma za jamii kama shule, pia ataziendeleza katika mkoa
huo kwa kuhakikisha kwamba zinajengwa shule kadhaa za kisasa, ambazo zitamudu
mahitaji ya watu wa eneo hilo.
Kwa upande wa huduma ya afya,
Sabodo alisema atatumia umaarufu wake kuwashawishi wamiliki wa Hospitali ya
kimataifa ya Apollo ya India ili waje nchini wakashirikiane naye kujenga
hospitali ya kisasa, ambayo itakuwa inatoa huduma za kisasa mkoani humo.
“Mnaifahamu hospitali ya Apollo ni
wawekezaji wakubwa katika huduma za afya, kwa kusukumwa na hatua hii ya Rais
nitaongea nao tushirikiane katika kujenga huduma za jamii katika mji huo,” alisema Sabodo.
Pia alisema atawashawishi
wawekezaji wengine kutoka nchi za India, Singapore na kwingineko kuja kuwekeza
katika mji huo wa Dodoma katika sekta ya viwanda, kuhakikisha kwamba azma ya
Rais Magufuli ya kujenga uchumi wa viwanda inatimia.
Sabodo ambaye alisema wazi kuwa
utendaji wa Rais Magufuli, umemvutia kutokana na hatua yake ya kupiga vita
rushwa, alitangaza kuwa kuanzia sasa hatatoa tena msaada kwa vyama vya upinzani
kama ambavyo amefanya miaka ya nyuma kama njia ya kuimarisha demokrasia nchini.
“Huko nyuma nilikuwa nawapa Chadema
fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kuimarisha demokrasia, sasa natangaza
tena kwamba sitawapa tena fedha, niwape za nini wakati Rais aliyeko madarakani
anafanya kazi ambayo ndio nilikuwa naipigania?" alihoji Sabodo.
Sabodo ni mfanyabiashara wa
kitanzania mwenye asili ya Kihindi ambaye alizaliwa mkoani Lindi. Katika maisha
yake amekuwa anafanya biashara katika nchi za Kenya, Ufaransa, India, Sudan na
Zimbabwe.
Pamoja na biashara zake, Sabodo
amekuwa anajihusisha kuchangia katika miradi ya maendeleo ya huduma za jamii,
uimarishaji wa demokrasia nchini na pia alishiriki kutunisha mfuko wa Taasisi
ya Mwalimu Nyerere kwa kuanzisha bahati nasibu.
No comments:
Post a Comment