MKUU wa Jeshi la Polisi nchini,
Inspekta Jenerali (IGP), Ernest Mangu, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Abdulrahman Kinana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju,
hawakutokea kwenye mkutano ulioandaliwa na Tume ya Haki na Utawala Bora jijini
Dar es Salaam jana.
Mkutano uliokuwa na lengo la kumaliza mvutano ulioibuka kati ya vyombo vya dola na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Mvutano huo unatokana na amri ya
Rais John Magufuli, ya kupiga marufuku kufanyika kwa maandamano na mikutano ya
vyama vya siasa hadi mwaka 2020.
Rais Magufuli, hata hivyo,
ameruhusu viongozi waliochaguliwa kama madiwani na wabunge kufanya mikutano
kwenye maeneo waliyopigiwa kura.
Kupinga amri hiyo, Chadema kimeamua
kuitisha maandamano na mikutano ya wanachama na wafuasi wao nchi nzima
yatakayofanyika, Septemba mosi, mwaka huu katika operesheni waliyoipa jina la
`Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania’ (Ukuta).
Baada ya kuibuka kwa mvutano huo,
uliosababisha Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu kukamatwa na Jeshi la
Polisi na kufunguliwa mashtaka ya uchochezi, tume hiyo iliwaita IGP Mangu,
Kinana, Masaju, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, Katibu Mkuu
wa Chadema, Vincent Mashinji na Mkurugenzi wa Taasisi ya Demokrasia (TCD),
Daniel Loya.
Hata hivyo, IGP Mangu, Kinana na
Masaju hawakuhudhuria mkutano huo kutokana na kile kilichoelezwa kuwa walitoa
udhuru.
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu
na Utawala Bora, Bahame Nyanduga, alisema jijini jana kuwa wametoa mapendekezo
matatu ambayo yanapaswa kufuatwa na pande zote zinazovutana.
Alisema mapendekezo yao yamelenga
kutoa nafasi kwa mahakama kuamua kesi zilizofunguliwa.
Nyanduga aliyataja mapendekezo hayo
kuwa ni Jeshi la Polisi na Chadema kusitisha matumizi ya lugha au maneno yenye
viashiria vya uvunjifu wa amani, haki za binadamu na utawala bora kwa kuwa
lugha hizo hazikidhi matakwa ya sheria.
Alisema wamependekeza Jeshi la
Polisi linapaswa kutokutumia maneno "tutawashughulikia wote watakaokaidi
amri" kwa kuwa tume inaamini kuwa matumizi ya maneno hayo yanaweza
kusababisha matumizi mabaya ya mamlaka ya jeshi hilo.
“Ni katika
mazingira haya, tume imepata wasiwasi kuwa endapo matamko haya yataachiwa
yaendelee, yana viashiria vya machafuko na uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu
unaoweza kutokea,” alisema Nyanduga.
Alisema pendekezo lingine ni
Chadema kurekebisha msamiati wa mikutano wanayopanga na kuondoa neno udikteta
katika mikakati yao ya kisiasa.
Akifafanua kuhusu pendekezo hilo,
Nyanduga alisema Tanzania ni nchi yenye taasisi za kidemokrasia na inaheshimu
utawala wa sheria na ndiyo sababu Chadema wamekwenda mahakamani.
Alisema Chadema na Jeshi la Polisi
wanapaswa kuheshimu mahakama na kuacha kutoa matamko ambayo yanaendelea
kuongeza joto kuhusu uwapo au kutokuwapo maandamano na mikutano ya Septemba
Mosi, mwaka huu.
Nyanduga alisema pendekezo la tatu
ni Chadema kusitisha maandamano yake ili kutoa nafasi kwa mahakama kufanya kazi
yake kwa umakini bila shinikizo la muda kuanzia sasa hadi Septemba Mosi.
Alisema kutozingatiwa kwa
mapendekezo hayo kutasababisha kutokea kwa uvunjifu wa haki za binadamu na
jambo hilo likitokea, wahusika wote watawajibishwa.
Alisema tume ina mamlaka ya
kujadili hoja hizo mbili kwa kuzingatia mamlaka iliyonayo chini ya Ibara 130
(1) (g) na (h) ya Katiba ya nchi, kuhusu kutoa ushauri na kutafuta maelewano
kati ya viongozi wa serikali na Jeshi la Polisi kwa upande mmoja na uongozi wa
Chadema.
Nyanduga aliongeza kuwa mkutano wa
jana ulikuwa na lengo la kuzungumzia tamko la Jeshi la Polisi la kuzuia
mikutano na maandamano ya vyama vya siasa isiyo ya kiutendaji na tamko la
Chadema kuhusu Ukuta.
“Ofisi ya AG, IGP
na CCM tuliwaalika, lakini walitujibu kuwa hawataweza kuhudhuria kwa kuwa wana
udhuru, hivyo tulikutana na Chadema, Ofisi ya Msajili na TCD (Kituo cha
Demokrasia Tanzania), na kukubaliana kutafanyika kikao kuhusu umuhimu wa
kudumisha amani nchini,” alisema Nyanduga.
Julai 27, mwaka huu, Mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe, alitangaza kuzinduliwa kwa Operesheni Ukuta kwa lengo
la chama hicho kufanya mikutano nchi nzima ifikapo Septemba Mosi mwaka huu,
baada ya amri ya Rais Magufuli na Jeshi la Polisi kuzuia kufanyika kwa mikutano
ya kisiasa na maandamano nchini.
Mashinji Afunguka
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk.
Mashinji, alipotafutwa ili kueleza juu ya mapendekezo ya tume, alisema
anashangaa kuambiwa kwamba kuna masuala yaliyojadiliwa kwa kuwa kikao
hakikufanyika jana.
“Mbona hicho kikao hakijafanyika?
"alihoji. "Kulikuwa na mvutano kwamba kifanyike ama
kisifanyike kwa sababu akidi haikutimia, nashangaa kusikia kuna maazimio
yamepitishwa.
“Hiyo inaonyesha
kabisa ni njama za hao watu ili ionekane kuna kikao kilifanyika, kikao
kisingeweza kufanyika kwa sababu hawakuwapo Kinana, IGP, wala AG,” alisema Dk.
Mashinji.
Alisema anachojua yeye ni kwamba,
wao wanaendelea kama kawaida na maandalizi yao ya mikutano ya hadhara na
maandamano nchi nzima hiyo Septemba 1, mwaka huu.

No comments:
Post a Comment