MMOJA wa madereva waliosababisha
ajali ya mabasi ya Kampuni ya City Boy iliyotokea Julai 4, mwaka huu na
kutoroka, Boniface Mwakalukwa (37), amejisalimisha mikononi mwa polisi na
kufikishwa mahakamani.
Mwakalukwa ambaye ni mkazi wa
jijini Dar es Salaam jana aliunganishwa kwenye mashitaka na dereva mwenzake
Jeremiah Semfungwe (34) wote kwa pamoja wakikabiliwa na makosa 30 ya kuua bila
kukusudia.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Singida, Joyce Minde ilidaiwa kuwa washitakiwa
hao walitenda makosa hayo Julai 4, mwaka huu saa 8.15 mchana wakati wakiendesha
mabasi aina ya Scania yenye namba za usajili T 247 BCD na T 331 DCE kwa
kuyagonganisha.
Ilidaiwa kuwa kitendo hicho ambacho
kilitokea Kijiji cha Maweni wilayani Manyoni kilisababisha vifo vya abiria 30
na majeruhi 54. Wakili wa Serikali, Petrida Muta alidai kuwa siku ya tukio
watuhumiwa wakiwa ni madereva wa Kampuni ya City Boys, bila kukusudia,
walisababisha vifo vya abiria hao kinyume na Kifungu 195 na 198 cha Kanuni ya
Adhabu Sura ya 16 Toleo la Kwanza.
Ingawa Wakili wa washitakiwa,
Francis Kitope aliiomba Mahakama iwape wateja wake dhamana kwa kuwa chini ya
Kifungu 148 cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kosa hilo linadhaminika, Wakili wa
Serikali Muta alipinga dhamana hiyo.
Muta ambaye aliwasilisha Hati ya Kiapo
mbele ya Mahakama hiyo, alidai kuwa kwa kufanya hivyo usalama wa washitakiwa
utakuwa hatarini kwa kuwa ndugu wa marehemu na majeruhi bado wana hasira
kutokana na ajali hiyo kuwa bado haijasahaulika.
Aidha, Muta aliendelea kudai kuwa
baadhi ya majeruhi wa ajali hiyo hali zao bado ni mbaya na hatma yao
haijulikani, hivyo si vyema washitakiwa kupewa dhamana wakati huu. Kutokana na
upelelezi wa kesi hiyo kutokamilika, washitakiwa wamerejeshwa rumande hadi
Agosti 4, mwaka huu kesi yao itakapotajwa tena.
No comments:
Post a Comment