Watu 14 wamefariki dunia katika wilaya za Chemba mkoani Dodoma
na Kiteto mkoani Manyara kutokana na ugonjwa unaojulikana kitaalamu kama
‘Aflatoxicosis’ unaosababishwa na sumu kuvu (Aflatoxins) kwenye nafaka
iliyoharibika.
Hayo yamesema na Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati akitoa taarifa
kwa waandishi wa habari juu ya magonjwa ya milipuko na magonjwa mengine leo
jijini Dar es Salaam.
“Ugonjwa uliosababishwa na sumu
kuvu (Aflatoxins) uliripotiwa kwa mara ya kwanza tarehe 13 Juni, 2016 katika
wilaya za Chemba mkoani Dodoma na baadaye mkoani Manyara katika wilaya ya
Kiteteo” alisema Waziri Ummy na kuongeza kuwa:
“Wagonjwa walikuwa na dalili za
kuumwa tumbo, kuharisha, kutapika, tumbo kuvimba na kuwa manjano sehemu
mbalimbali za mwili ambayo inaashiria kuathirika kwa ini”
Alisema mbali na vifo hivyo, hadi
kufikia Julai 31 mwaka huu wagonjwa 54 waliripotiwa kuugua ugonjwa hu huku
wagonjwa wanne wakilazwa kutokana na kuugua.
“Hadi kufikia tarehe 31, July 2016
kulikuwa na wagonjwa 54 na watu 14 walipoteza maisha kutokana na ugonjwa
huo.Aidha katika wiki iliyopita aliripotiwa mgonjwa mmoja mpya kutoka wilaya ya
Kondoa” alisema Waziri Ummy na kufafanua kuwa:
“Jumla ya wagonjwa waliolazwa
wodini ni wanne kati yao mmoja yupo Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na watatu wapo
katika Hospitali ya Kondoa”
Waziri Ummy alitaja wilaya
zilizoripoti wagonjwa hao na idadi ya wagonjwa kuwa ni wilaya ya Chemba
wagonjwa 38, Kondoa wagonjwa tisa , Kiteto wagonjwa watatu, Chamwino wagonjwa
wawili na Dodoma Manispaa mgonjwa mmoja.
“Vijiji vilivyoathirika zaidi na
ugonjwa huo ni kutoka wilaya ya Chemba ambavyo ni Kinkima, Itolwa, Mwailanje na
katika wilaya ya Kondoa ni kijijini cha Ubembeni” alisema
Waziri Ummy.
Hivyo, aliitoa hofu familia
iliyopoteza watu wanne katika kijiji cha Mwaikuzabe na kusema vifo hivyo
havihusiani na uchawi au kuwekewa sumu bali ni chakula cha siku ile
kilithibitika kwamba kilikuwa na sumukuvu.
Kufuatia athari hizo Serikali
itafanya uchunguzi wa kina katika wilaya kumi za Chemba, Kondoa, Chamwino
na Kiteto na wilaya nyingine za mikoa ya Sindida, Dodoma na Manyara
zinazopakana na wilaya hizo.
Alisema uchunguzi huo unalenga
kubaini hali ya usalama wa vyakula vinavyotumiwa na jamii ili kuzuia kuenea kwa
ugonjwa huo na kuwaathiri wananchi wengi zaidi wanaoishi katika wilaya hizo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taifa
wa Afya wa Wizara hiyo Dkt. Fausta Mosha alisema wizara imeandaa
vipepereshi vyenye maelekezo yanayotoa elimu juu ya kijikinga kwa kuandaa
chakula kuanzia hatua ya uvunaji shambani hadi wakati wa kula.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali
Dkt. Otilia Gowelle alisema njia bora ya kupambana na ugonjwa huo ni kuukinga
kwa kuhakikisha sumu kuvu haizalishwi kutoka kwenye nafaka.
Akifafanua kuhusu udhibiti, Waziri
Ummy alisema wanashirikiana na Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi kutoa elimu kwa
wananchi juu ya njia sahihi ya uhifadhi na uandaaji wa chakula utakaosaidia
kupunguza kiasi cha sumukuvu kwa nafaka ambazo hazijaharibika sana.
“Njia hizi ni pamoja na kuhifadhi
nafaka zilizokauka vizuri na kuchambua nafaka zilizoharibika (zilizooza,
kuvunjika, zilizobadilika rangi), kukoboa mahindi kabla ya kusaga au kuacha
kutumia nafaka zitakazoonekana kuharibika rangi” alisema.
Waziri Ummy alisisitiza Serikali
kuendelea kuimarisha mikakati ya kitaifa ya kupunguza uchafuzi wa sumukuvu
katika vyakula, ikiwa ni pamoja na kujenga uwezo wa kupima sumukuvu katika damu
na choo kidogo miongoni mwa taasisi za ndani ya nchi.
Inaelezwa kuwa ugojwa
wa‘Aflatoxicosis’unaosababishwa na sumu kuvu (Aflatoxins) kwenye nafaka uliwahi
kutokea nchini Kenya mwaka 2004 na kusababisha vifo vya zaida ya watu 100 huku
wengine 200 waliathirika.
No comments:
Post a Comment