
SIKU mbili baada ya Spika wa Bunge,
Job Ndugai kuahidi kufanyika maridhiano kati ya uongozi wa Bunge na wabunge wa
upinzani katika kikao kijacho kinachotarajiwa kuanza Septemba 6, mwaka huu,
Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson amesema hataki kuwasikia wabunge wa upinzani wala
kuwawaza.
Kauli hiyo ya Naibu Spika huenda
ikazidi kutonesha kidonda hasa baada ya Bunge la Bajeti lililofanyika Mei mwaka
huu kuacha majeraha kutokana na wabunge wa upinzani wanaounda Umoja wa Katiba
ya Wananchi (Ukawa), kususia vikao vyote vilivyoendeshwa na kiongozi huyo.
Juzi wakati akihojiwa kupitia
kipindi cha Funguka kinachorushwa na Kituo cha Luninga cha Azam, Spika
Ndugai, alisema anatafuta mbinu ya kuweka sawa mambo hayo kwa kufanya
maridhiano ikiwemo kushirisha maspika wastaafu.
Akizungumza na gazeti la Mtanzania
juzi katika mahojiano maalumu ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Dk. Tulia
alisema hapendi kuwawazia wabunge hao wa upinzani.
“Kwa kuwa Spika yeye kazungumza
siwezi kucomment chochote kwa sababu sipendi kuwawazia wabunge hao,”alisema.
Alipoulizwa kwamba ni kwanini
migogoro ilizidi wakati yeye akiwa anaendesha vikao, alisema alichokuwa
anafuata ni kanuni na kwamba malalamiko hayawezi kukosekana.
“Nashangaa wengine wanasema
kuendesha vikao ni mpaka uwe na uzoefu…unajua zile kanuni hata ukipewa uendeshe
wewe ukishazielewa hazihitaji uzoefu wowote. Kulalamika kuwa nawapendelea ni
jambo la kawaida.
“Kwa mfano siku iliyotokea vurugu
wakati wabunge wa upinzani wanadai kutorushwa matangazo ya Bunge live,
aliyekuwepo kwenye kiti alikuwa ni mwenyekiti ambaye ni mzoefu wa siku nyingi
na ni yeye aliyepeleka majina yao kwenye Kamati ya Maadili, sasa sidhani kama
hiyo ni hoja,”alisema Dk. Tulia
Alieleza kushangazwa kwa kitendo
cha wabunge wa upinzani katika barua yao waliyomwandikia Spika kwamba hawana
imani naye, huku akihusishwa na fedha zilizorejeshwa serikalini.
“Katika ile barua walieleza sababu
nyingine kuwa hawana imani na mimi, wakanihusisha na zile Shilingi bilioni 6
zilizorejeshwa serikalini wakati sheria na utaratibu upo wazi kwa sababu Spika
au Naibu Spika hauhisiki na masuala ya fedha bali anayehusika ni Katibu wa
Bunge.
“Kwa hiyo ni jambo la kushangaza
kwamba Naibu Spika karudisha fedha, mimi si mshika mafungu lakini pia ni namna
watu walivyopokea huwezi kuwazuia wanavyokuwazia,” alisema.
Akizungumzia kauli ya Spika Ndugai
kwamba kwa kuwa Bunge la 11 lina wabunge wapya wengi na kwamba kuwaongoza
kunahitaji uvumilivu mkubwa alisema: “Nisingependa kuongelea kauli ya
Spika…lakini uvumilivu wa mtu kutakiwa akae hadi mara 11 halafu ameendelea kusimama
ni uvumilivu gani huo?,” alihoji.
Pamoja na mambo mengine alisema
wakati wabunge wanawake wa Ukawa walipojitoa kwenye Chama cha Wabunge
Wanawake (TWPG), alitukanwa tusi kubwa lakini alinyamaza.
Mei 5, mwaka huu wakati akichangia
mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Katiba na
Sheria, Mbunge wa Ulanga Mashariki, Gudluck Mlinga (CCM), alidai kuwa ili kuwa
mbunge wa viti maalumu Chadema lazima uwe ‘baby’ wa mtu.
“Laiti ungeona Hansard tusi
walilonitukana siku ile, actually Mlinga hajatukana lakini ulisikia
nikilalamika mahali kwamba nimetukanwa? wao wanaongee vibaya…watukane, mimi
bado ni kiongozi wao na siwezi kuanza kuwakasirikia itakuwa sasa nashindwa
kuwaongoza mimi ni kama mzazi wao,” alisema Dk. Tulia.
Alisema kitendo cha watu kudai
kwamba anafanya upendeleo bungeni ni changamoto ya kawaida, kwa sababu hata
katika mabunge ya Jumuiya ya Madola malalamiko ya aina hiyo yapo.
“Pale bungeni wako wabunge
389, hawa ni wengi sana wote hawawezi kupata nafasi ya kuongea. Kwa mfano
uliomba nafasi jana ukapewa ukaomba leo, hata ukisimama mara 11 katika hali ya
kawaida huwezi kupewa kwa sababu wako wengi ambao hawajachangia.
“Kama kiongozi naona ni sehemu
mojawapo ya kusimamia jamii ni changamoto na itaendelea kuwepo kwa miaka
mitano,”alisema Dk. Tulia.

No comments:
Post a Comment