
Polisi wamewatia mbaroni watu
watano wanaodaiwa kusambaza taarifa kwenye mitandao ya jamii kuwa Mbunge
wa zamani wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo amefariki dunia.
Miongoni mwa waliokamatwa na
kuhojiwa na polisi na simu zao kushikiliwa kwa uchunguzi, ni wanachama wa
Chadema na maofisa wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia).
Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro,
Wilbroad Mutafungwa jana alisema kuwa, uzushi huo kuwa Ndesamburo
amefariki dunia, ulisambazwa zaidi kupitia makundi ya WhatsApp.
“Tarehe 29/7/2016 mzee Ndesamburo
alifika polisi na kutoa taarifa kuwa katika mitandao ya jamii kuna taarifa na
picha yake, inasambazwa kwa kasi kuwa amefariki dunia,” alisema
Mutafungwa na kuongeza:
“Picha hiyo ilikuwa na maneno RIP
(Rest in Peace), wakimaanisha apumzike kwa amani. Tulifungua jalada na kitengo
chetu cha Cyber Crime (makosa ya kimtandao) kiliingia kazini.”
Alisema watu mbalimbali walihojiwa
na polisi wanaendelea kazi hiyo pia watu watano walikiri kupokea ujumbe huo na
kuusambaza.
Kamanda Mutafungwa alisema
wanaendelea na uchunguzi wa kisayansi kumpata mtu aliyeanzisha ujumbe huo,
ambao ulisababisha usumbufu kwa Ndesamburo na familia yake.
Wanaoendelea kuhojiwa ni Ofisa
Usalama wa Kampuni ya Kilimanjaro Airport Development (Kadco) na msimamizi wa
waongoza ndege wa Fast Jet Uwanja wa Kia.
Wengine ni wanachama watatu wa
Chadema, ambacho Ndesamburo ni Mwenyekiti wake wa Mkoa Kilimanjaro. Katibu wa
Chadema Mkoa Kilimanjaro, Basil Lema alithibitisha kuhojiwa kwa wanachama wake
na kwamba, anaamini mwanzilishi wa taarifa hiyo ya uzushi hajakamatwa.

No comments:
Post a Comment