Mbunge wa Arusha Mjini, Goodbless
Lema amemvaa Mkuu wa wilaya hiyo, Mrisho Gambo mbele Naibu Waziri Nchi, Ofisi
ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Suleiman Jaffo akidai
anaingilia shughuli za halmashauri kinyume na taratibu.
Lema alimtuhumu Gambo kutoheshimu
mipaka yake ya kiutawala kwa kuingilia maamuzi ambayo yamejadiliwa kwenye vikao
halali vya halmashauri na kupitishwa na ofisi ya mkuu wa mkoa katika kikao cha
wakuu wa idara, maofisa tarafa, waratibu wa elimu kata watumishi wa Mamlaka ya
Majisafi na Majitaka (Auwsa).
“Nimeona nizungumze hapahapa ili
naibu waziri ufahamu hali ilivyo hapa. Kwa mfano, Baraza la Madiwani lililopita
ndilo lililopitisha kiwango cha posho kwa madiwani kutoka Sh100,000 hadi
Sh120,000, jambo la kushangaza DC ameandika barua Tamisemi na nakala kwa
Takukuru ili wachunguze jambo ambalo limeshapata baraka za Tamisemi,” alisema Lema.
Alisema pia amekuwa akiingilia
utendaji wa watumishi wa halmashauri kwa kuingilia upangaji wa vibanda vya
wafanyabiashara kupitia madalali na kusababisha usumbufu.
Lema aliongeza kuwa Gambo pia
amekuwa akitaka uwanja ulionunuliwa na mfanyabiashara urudishwe Jiji wakati
kesi imempa uhalali aliyenunua kuchukua eneo hilo.
Hali hiyo ilimfanya naibu waziri
kuingilia kati na kuahidi kuzishughulikia changamoto hizo na kumpa nafasi Gambo
kujibu madai ya Lema ambayo aliyakanusha, likiwamo la kuingilia utendaji kazi
wa mamlaka ya maji.
“Mheshimiwa mbunge nataka ujue mimi
ndiyo mkuu wa shughuli za Serikali hapa wilayani, muda wowote nina uwezo wa
kuingilia kati mambo ambayo naona hayaendi sawa hata kama yupo katibu tawala na
viongozi wengine.
"Rais aliona ninafaa, ndiyo
maana akaniteua na sihitaji kujifunza namna ya kuwa mkuu wa wilaya, huu ni
mwaka tano,” alisema.
Alisema hakuna siasa kwenye
maendeleo ya wananchi na kumtaka mbunge atambue kuwa kuhudumia wananchi
hakuhitaji maamuzi ya Baraza la Madiwani pekee, kwani kumekuwa na tabia ya
kutumia fedha za halmashauri vibaya kulipana posho ambazo hazipo kwa mujibu sheria
na kanuni.
Alisema alilazimika kutaka viongozi
walio chini yake kupitia hukumu iliyompa mfanyabiashara eneo la Kilombero kama
ni halali na kushangazwa na Lema kupinga.
Akizungumzia suala hilo, Jaffo
alimtaka Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega kushughulikia changamoto
hizo akisema muda wa siasa umepita na wananchi wanahitaji maendeleo.
Pia, alisema Serikali ipo mbioni
kuwahamisha watumishi wa halmashauri ya jiji wanaofanya kazi kwa mazoea na
kumwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Athuman Kihamia
kusimamia wafanyakazi wanaofanya kazi kwa mazoea huku wananchi wakipata shida.
No comments:
Post a Comment