Na Tiganya Vincent
Wasomi na Wanazuoni mbalimbali
wamepongeza hatua ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John
Pombe Magufuli na Waziri Mkuu zamani Edward Lowassa kushikana mikono na
kusalimiana wakati wa Jubilei ya dhahabu ya miaka 50 ya ndoa ya Rais Mstaafu
Benjamin William Mkapa na Anna Mkapa.
Wanazuoni hao wametoa kauli
hiyo jana katika mahojiano maalum na Idara ya Habari iliyokuwa ikitaka kupata
maoni yao kuhusu kitendo kilichoonyeshwa na viongozi hao kwa jamii.
Profesa Kitila Mkumbo wa Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam alisema kuwa hatua hiyo imeonyesha kuwa huo ndio Utanzania
ulivyo wa kutofautiana bila kugombana.
Alisema kuwa kitendo hicho
kimewaonyesha wananchi kuwa mazungumzo yana nafasi kubwa ya kuondoa tofauti
zilizopo kuliko kutumia njia nyingine kama vile maandamano na mabavu katika
kutafuta ufumbuzi wa baadhi ya matatizo.
“Kukutana kwa viongozi hao na kupeana
mikono wakati wa kusalimiana kunakumbusha utamaduni wetu uliojingekea toka siku
nyingi wa kutatua matatizo yetu kwa mazungumzo bila kugombana au kutumia
mabavu,”alisema Profesa Mkumbo.
Kwa upande wa Profesa Joseph
Semboja alisema kuwa amefurahishwa sana na kitendo kilichoonyeshwa na viongozi
hao kwani kimeuonyesha ulimwengu kuwa Watanzania ni watu wenye Amani na
upendo.
Alisema kuwa hatua hiyo imeonyesha
kuwa Watanzania wanaweza kuwa na tofauti lakini wakaendelea kuishi pamoja na
kushirikiana katika mambo mbalimbali ya kijamii kwa ajili ya maendeleo yao na
Taifa lao.
Profesa Semboja aliwataka wananchi
kujifunza kutokana na kitendo kilichoonyeshwa na viongozi hao ambao wameonyesha
kuwa ni lazima wakae pamoja kwa ajili kushughulikia mambo muhimu ya maendeleo
ya wananchi badala kuendeleza tofauti ambazo hazina manufaa kwa Watanzania.
Alisema kuwa ipo haja ya kwenda
zaidi ya hapo kwa kuweka utaratibu wa kukaa pamoja na kujadiliana ili kutatua
vyanzo vya migogoro kwa ajili ya mustakabali mzuri wa Taifa hili.
Profesa alisema kuwa sio sahihi
kutumia mfumo wa jino kwa jino kwani utaratibu huo ndio unaoweza kusababisha
kukua zaidi kwa migogoro na wakati mwingine unasababisha umaskini kwa wananchi
na Taifa kwa ujumla kwani muda mwingi wananchi hawana muda wa kushiriki katika
shughuli za maendeleo kwa sababu ya migogoro.
Naye Profesa Samwel Wangwe alisema
kuwa hatua ya viongozi hao kukutana na kupeana mikono ni ishara kwa Watanzania
kujifunza kuwa mazungumzo yana nafasi kubwa katika kuleta muafaka mgogoro
wowote kuliko kutunishiana misuli.
Alisema kuwa mazungumzo yana nguvu
kubwa katika kuleta upatanishi katika migogoro mbalimbali inatokea katika jamii
kuliko kutumia njia nyingine ambazo zinaweza kusababisha vurugu na uharibifu wa
mali za watu na upotevu wa maisha ya watu.

No comments:
Post a Comment