
Spika wa zamani wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Pius Msekwa amewaasa watanzania kuacha kufuata mkumbo wa kisiasa badala yake
watii mamlaka ili kuepuka kuvunja sheria na kuleta madhara kwao binafsi na
taifa kwa ujumla.
Msekwa aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati
akizungumzia masuala mbalimbali kuhusu mwenendo wa siasa za hapa nchini na
utendaji kazi wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. John
Pombe Magufuli. Alieleza kuwa watu wengi wana hulka ya kufuata mkumbo kwenye
mambo fulani bila ya kuchunguza na kufahamu ukweli wake kabla ya kushabikia.
“Ni hulka ya watanzania kushabikia mambo wasiyoyafahamu ilimradi
tu yanawafurahisha masikioni au machoni mwao kwani hata huko
mitaani wanakimbilia ngoma bila ya kujua inatokea wapi au inaelekea wapi, hivyo
nawasihi wajaribu kuwa makini na mbinu za siasa zinazotumiwa na baadhi ya vyama
kwa kuwa nyingine zina madhara ndani yake.” Alisema Msekwa.
Akifafanua mwenendo wa siasa za hapa nchini, Mzee Msekwa alisema
kuwa bado wanasiasa wengi hawafuati kanuni za ushindani wa kisiasa katika
kutafuta madaraka badala yake wanatumia mbinu ambazo zinavunja sheria za nchi
na hatimaye wanapambana na mamlaka.
“Ushindani wa kisiasa ni jambo la kawaida na linalokubalika
ingawa ushindani huo ni lazima ufuate sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa
ili kufikia lengo, hivyo kubuni vitu ambavyo vinachochea utovu wa nidhamu na
uvunjifu wa amani sio jambo zuri, ' alisisitiza.
Aidha, Msekwa alieleza kuwa utendaji wa Mhe. John Magufuli ni wa
kuridhisha na wa aina yake kwa kuwa amekusudia kuleta mabadiliko chanya kwa
watanzania na kuondoa mfumo wa utendaji kazi kwa mazoea jambo ambalo limesaidia
kurudisha nidhamu kwa watumishi wa Serikali.
Akizungumzia uzoefu wake katika masuala ya kuongoza Bunge,
alieleza kuwa tofauti ya Bunge la zamani ni kwamba lilikuwa na nidhamu kubwa na
linaheshimika lakini Bunge la sasa halina utii na hicho ndio chanzo cha
malumbano yanayojitokeza mara kwa mara katika vikao vya Bunge.
Aliongeza kuwa tangu awali wapinzani kazi yao ni kuipinga
Serikali iliyo madarakani lakini kwenye Bunge la uongozi wake walikuwa
wakipinga kwa kutumia hoja na kufuata kanuni bila ya kudharau mamlaka ya Spika
wala Serikali iliyoko madarakani.
“Kanuni zinatoa nafasi kwa mbunge asiyeridhika na maamuzi ya
Spika kushitaki kwenye Kamati ya Kanuni za Bunge, na kamati hiyo itasikiliza na
kutoa uamuzi kama mahakama inavyosikiliza lakini wabunge wa sasa hawataki
kutumia utaratibu bali hutumia mbinu za tofauti ili waweze kupata sifa ambazo
hazina tija kwa wananchi waliowachagua,” alisema.
Msekwa pia amewaasa vyama vya upinzani kutumia mbinu nzuri
katika kutafuta madaraka bila ya kuvunja sheria au kuhatarisha amani ya nchi
kwani waliowachagua wanategemea zaidi matokeo ya kazi waliyoahidi kuwatumikia
kuliko malumbano yasiyo na tija kwa ustawi wao na taifa.
mwisho

No comments:
Post a Comment