
Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA imewataka
wafanyabiashara katika jiji la Dar es salaam kuboresha taarifa za usajili wa
namba ya utambulisho wa mlipa kodi (TIN) ili kuondokana na mfumo wa kizamani wa
usajili wa namba hiyo.
Uhakiki huo utaiwezesha mamlaka
hiyo kuweza kujua idadi sahihi ya wafanyabiashara walipa kodi, kuondoa walipa
kodi hewa ambao wamekuwa hawajihusishi na biashara kutokana na sababu
mbalimbali ikiwemo vifo au kufungwa kwa makampuni yao.
Akiongea na waandishi wa habari
jana jijini Dar es salaam, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania ndugu
Alphayo Kidata alisema mfumo huo utawawezesha wafanyabiashara kulipa kodi kwa
gharama nafuu sambamba na kuweka mazingira ya ulipaji kodi kwa hiari.
Kidata alisema kuwa mfumo wa sasa
wa uhifadhi kumbukumbu za walipa kodi ulikuwa na kasoro nyingi hivyo mfumo mpya
utaendana na ukuaji wa teknolojia na kukuza uchumi.
“Zoezi hili linamtaka kila mwenye
namba ya utambulisho yani TIN kufika katika ofisi za TRA zilizopo karibu naye
bila kuwakilishwa na mtu yeyote na zoezi litatumia dakika 10 kumalizika” alisema
Naye Elija Mwandubya ambaye ni
kamisha wa mapato wa ndani wa mamlaka hiyo, alisema zoezi hilo litachukua siku
60 na kuanzia Dar es salaam na baadaye kuhamia mikoa mingine ndani ya nchi.
“TRA ina wafanyabiashara walipa
kodi milioni mbili na laki moja hivyo uboreshwaji wa TIN utatupa uelewa wa
idadi kamili ya walipa kodi”Alisema
Elija alisema kutakuwa na vituo
maalum kwaajili ya uhakiki wa taarifa katika mikoa ya kikodi ambapo Kinondoni
wafanyabiashara watatakiwa kutembelea ofisi za TRA zilizopo jengo la LAPF –
Kijitonyama na Kibo Complex Tegeta.
Ilala wafanyabiashara watembelee
ofisi ya TRA shauri moyo na 14 Rays Gerezani na Temeke wafike ofisi za uwanja
wa Taifa.

No comments:
Post a Comment