WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto imewataka wananchi na wadau kutoa taarifa, iwapo kuna
mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) zinazojihusisha na kuhamasisha vitendo
vya ushoga nchini ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi ya taasisi hizo.
Agizo hilo lilitolewa jana jijini
Dar es Salaam na Msajili wa NGOs, Marcel Katemba. Alisema kuwa siku za hivi
karibuni, kumekuwepo na tuhuma za kuwepo kwa baadhi NGOs kujihusisha na
kuhamasisha vitendo vya ushoga nchini.
Alisema ni vyema jamii ikatambua
kuwa NGOs zinasajiliwa kwa lengo la kutekeleza majukumu yanayokubalika kisheria
na kwamba vitendo vya kuhamasisha ushoga si majukumu halali yanayopaswa
kutekelezwa.
“Tunazitaka NGOs kutekeleza
majukumu yaliyo ndani ya usajili wao na kuepuka vitendo vya uvunjifu wa sheria
kwani kinyume na hayo hatua zitachukuliwa,” alisema Katemba na kusisitiza
kuwa vitendo vya ushoga havikubaliki nchini kwani ni kinyume na mila, desturi
na sheria za nchi.
Alisema katika kudhibiti uwepo wa
vitendo hivyo, wadau na umma kwa ujumla wanapaswa kutoa taarifa zitakazowezesha
kuthibitisha tuhuma hizo ili hatua kali zichukuliwe kwa wahusika.
Katemba alisema taifa lina mila,
desturi na sheria za nchi ambazo imekuwa ikizisimamia na kuzitekeleza na
kuhamasishwa kwa vitendo hivyo kunakwenda kinyume na misingi, ambayo kwa namna
moja vinaweza kuathiri kizazi kwa kizazi.
Alisema ni wakati sasa kwa kila NGO
kusimamia utekelezaji wa majukumu yake kama ilivyosajiliwa, kuongeza ushiriki
wake kwa kutoa michango yao katika kuleta maendeleo kwa jamii.
Alisema taratibu za usajili wa NGOS
chini ya sheria mashirika yasiyo ya kiserikali namba 24 ya mwaka 2002,
yameimarishwa vyema na kila shirika linalokuwa limepata usajili ni muhimu
kutekeleza yale yaliyokusudiwa ili kuepuka taifa kuingia katika vitendo
visivyostahili.
No comments:
Post a Comment