Waziri wa Elimu, Prof. Joyce Ndalic hako
MWALIMU Daniel Msalika (42) wa
shule ya msingi Nyasosi, wilayani Bariadi, mkoa wa Simiyu amefariki dunia
katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando alikokuwa amelazwa akitibiwa majeraha.
Majeraha hayo yalitokana na
kushambuliwa na baadhi ya wananchi kwa madai ya kujihusisha kimapenzi na
wanafunzi wa kike wa shule hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu,
Onesmo Lyanga aliwaeleza waandishi wa habari jana ofisini kwake kuwa mwalimu
huyo alifariki dunia Julai 31 mwaka huu saa nane usiku.
Kamanda Lyanga alisema kuwa siku ya
tukio Julai 27 mwaka huu saa 6.30 usiku, wananchi hao ambao idadi yao
haijafahamika, walivamia nyumba ya mwalimu huyo baada ya kupata taarifa kuwa
kuna mwanafunzi ambaye amelala nyumbani kwake, jambo ambalo halikuwa la kweli.
“Wananchi hao walipata taarifa ya
kuwa nyumbani kwa mwalimu kuna mwanafunzi ambaye amelala humo hivyo walimvamia
kwa kuvunja mlango na kuanza kumshambulia kwa kutumia silaha mbalimbali za jadi
na kumsababishia majeraha makubwa sehemu za kichwani na usoni lakini binti
waliyemkuta kwake ni mwenye umri wa miaka 18 na siyo mwanafunzi,” alisema.
Alisema kuwa baada ya uvamizi huo,
mwalimu huyo alikimbizwa katika Kituo cha Afya cha Isanga kupatiwa matibabu,
lakini hali yake iliendelea kuwa mbaya na kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa
ya Bugando jijini Mwanza, lakini alifariki dunia.
Kamanda alisema kifo chake,
kimesababishwa na majeraha ya kushambuliwa huku tuhuma dhidi yake zikiwa si za
kweli.
Alitoa mwito kwa wananchi kuacha
kujichukulia sheria mikononi huku wakisisitiza kuwa wote watakaobainika
kusababisha kifo hicho, sheria itachukua mkondo wake.
No comments:
Post a Comment