Madiwani wa Ukawa wa Manispaa ya
Kinondoni wamesusa kikao kilichoitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda kwa madai kiongozi huyo hana uhusiano mzuri na viongozi wa
upinzani.
Jana, Makonda aliitisha kikao cha
wakuu wa wilaya, wakurugenzi, wakuu wa idara za manispaa za Temeke, Ilala na
Kinondoni na madiwani wote, wakiwamo wabunge wanaounda halmashauri hizo.
Kikao hicho kilichofanyika kwenye
ukumbi wa mikutano wa Arnaoutoglou kililenga kuzungumzia masuala mbalimbali,
kama maeneo yaliyovamiwa na uboreshaji wa elimu mkoani Dar es Salaam.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake,
meya wa Kinondoni, Boniface Jacob alisema Makonda amekuwa na tabia ya kudharau
na kutoheshimu viongozi wenzake, hasa wa upinzani akiwaona hawatendi kazi
vizuri.
Pia, Jacob alidai kuwa Makonda
amekuwa na tabia ya kuingilia kazi zinazofanywa na viongozi wengine kwa kutumia
cheo cha ukuu wa mkoa, jambo ambalo meya huyo alisema ni kinyume cha
sheria.
“Akitaka tumpe ushirikiano, Makonda
abadilike la sivyo mtindo utakuwa huuhuu, mambo yatakuwa hivi. Huu ni mwanzo na
ndiyo maana leo (jana) Ukawa Kinondoni tumekuwa na msimamo mmoja,” alisema
Jacob.
Jacob, ambaye pia ni diwani wa
Ubungo (Chadema), alisema hawakuona umuhimu wa kwenda katika kikao hicho kwa
sababu kiongozi wa mkutano huo anawadharau.
Akijibu tuhuma hizo, Makonda
alisema madiwani waliohudhuria kikao hicho maeneo yao yalikuwa na shida na
yanahitaji kushughulikiwa, hivyo si kazi yake kuhesabu watu na kubaini nani
hakufika mkutanoni.
Alisema ajenda kuu ya kikao hicho
ilikuwa ni kujadiliana namna bora ya kuvirudisha viwanja vilivyochukuliwa na
kuvirejesha kwa matumizi yaliyokusudiwa.
“Huyo anayelalamika mwambie huo
anaoufanya ni utoto akikua ataacha. Narudia tena siyo kazi yangu kuangalia nani
hajaja kwenye kikao,” alisema.
Kwenye kikao hicho, meya wa Ilala
(Chadema), Charles Kuyeko alikuwapo kwenye mkutano huo pamoja na madiwani wenzake,
sambamba na wale wa Temeke.
Makonda si mgeni wa tuhuma
.Aliteuliwa kuwa mkuu wa wilaya ya Kionondoni katika kipindi ambacho alikuwa
akituhumiwa kuhusika kwenye sakata la kupigwa kwa Waziri Mkuu wa zamani, Jaji
Joseph Warioba kwenye mdahalo wa Katiba uliofanyika Hoteli ya Blue Pearl.
Katika kipindi hicho, Makonda pia
alikuwa akituhumiwa kumrushia tuhuma za ufisadi Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa akiahidi kuwa CCM isingempitisha kugombea urais.
Akitoa majumuhisho ya kikao cha
jana kilichoanza saa 2:00 asubuhi hadi saa 5:00 asubuhi, Makonda aliwataka watu
waliovamiwa na kujenga kwenye maeneo yasiyoruhusiwa, kuanza kubomoa majengo yao
kabla ya Serikali kuwafikia.
Kabla ya kutoa majumuisho hayo, Makonda
alitoa nafasi kwa madiwani wa manispaa hizo kueleza kero zinazowakabili,
hususan zinazohusu ardhi.
“Najua mchakato huu utawagusa hadi
vigogo, lakini mimi siogopi vita kwa sababu ndani yangu ninaongozwa na Mungu
pekee,” alisema Makonda.
Mbali na hilo, Makonda alisema
endapo mtendaji wa ardhi atayebainika kuhusika katika kuchezea michoro na
ramani ili aachie ardhi na kujipatia fedha, atashughulikiwa kwa mujibu
sheria.
Katika hatua nyingine, Makonda
amemwagiza kamishna msaidizi wa ardhi wa Kanda ya Dar es Salaam, Mathew Nhange
kumwambia Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
awaondoe maofisa ardhi na mipango miji wa Kinondoni na Ilala baada ya kushindwa
kutoa taarifa za kuridhisha katika mkutano huo.
Huku akiwataja maofisa hao
wanaotoka Kinondoni na Ilala, Makonda alisema alishakutana na wakuu wa idara
kwenye vikao vilivyopita, hivyo alitegemea kuwa watumishi hao wangetoa taarifa
zilizokamilika.
“Kamishna naomba umwambie katibu
mkuu mimi siwataki watumishi hawa katika manispaa hizi. Mwambie awatoe na
kuwapangia kazi nyingine,” alisema Makonda.
Kamishna Nhange alisema agizo hilo analifanyia kazi na kwamba atampa katibu mkuu taarifa za watumishi hao jana.
Kamishna Nhange alisema agizo hilo analifanyia kazi na kwamba atampa katibu mkuu taarifa za watumishi hao jana.
No comments:
Post a Comment