
MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless
Lema (Chadema), ameendelea kugoma kula kwa siku ya tatu mfululizo tangu
alipokamatwa Oktoba 26 mwaka huu, nyumbani kwake mjini hapa, akidaiwa kutoa
maneno ya uchochezi.
Lema alikamatwa siku hiyo saa 12
alfajiri akiwa nyumbani kwake, Njiro, na hadi sasa anashikiliwa katika
mahabusu ya kituo kikuu cha polisi mjini Arusha.
Kutokana na kuendelea kugoma kula,
Wakili wake, John Mallya amesema leo saa sita mchana atakwenda Mahakama Kuu,
Kanda ya Arusha kufungua kesi ya kutaka mteja wake afikishwe mahakamani.
Malya jana alisema katika kesi hiyo
atashirikiana na Chadema kuwashtaki mwendesha mashitaka mkuu wa Serikali na
mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai, Mkoa wa Arusha.
Tangu mbunge huyo akamatwe amegoma
kula kwa kile anachodai kupinga udhalilishwaji aliofanyiwa na polisi
wakati wa kukamatwa.
Pia, Lema anasema alinyanyaswa
mbele ya watoto wake nyumbani kwake huku wakijua yeye ni kiongozi na
amechaguliwa na wananchi.
Neema, mkewe Lema,jana
alithibitisha kwamba mumewe amegoma kula.
“Anaendelea kugoma kula mpaka sasa
kwa sababu hata sasa nimetoka polisi asubuhi kumpelekea chakula, lakini
amekataa kula.
“Lakini nilipouliza pale polisi
kuwa wanampeleka lini mahakamani, nilijibiwa wanaendelea kumhoji,”alisema Neema.
Juzi, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa
Arusha, Charles Mkumbo, alithibitisha kukamatwa kwa Lema na kueleza kuwa
alihojiwa dhidi ya matamshi ya uchochezi na kuwa atafikishwa mahakamani baada
ya kukamilika uchunguzi.
Kwa mujibu wa Kamanda Mkumbo, Lema
anatuhumiwa kuwachochea wakazi wa Arusha kuandamana Septemba mosi, mwaka huu
kuhamasisha kile kinachoitwa Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta).

No comments:
Post a Comment