
Chama Cha Wananchi (CUF)
kimewasimamisha uanachama aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim
Lipumba na Katibu Mkuu wa chama hicho upande wa Bara, Magdalena Sakaya.
Uamuzi huo umetolewa jana na Baraza
Kuu la Chama hicho lililofanya mkutano wake visiwani Zanzibar kwa lengo la
kuwajadili wanachama kadhaa wakiwemo vigogo hao. Sakaya amevuliwa nyadhifa zote
ndani ya chama kabla ya kusimamishwa.
Taarifa kutoka ndani ya Mkutano huo
zimeeleza kuwa Baraza hilo limewaadhibu wanachama 15 wakiwemo Sakaya ambaye pia
ni mbunge wa Kaliua.
Mbali na vigogo hao, wengine
waliopigwa rungu na Baraza Kuu la CUF ni pamoja na Katibu wa Baraza la Wazee,
Shashi Lugeye, Thomas Malima na Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano,
Abdul Kambaya.
Aidha, Baraza hilo limemsimamisha
uanachama Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftah Nachuma. Hatua hii inaweka matatani
ubunge wa Sakaya na Nachuma kwani wakifikia hatua ya kufukuzwa watakosa sifa za
kuendelea kuwa wabunge.
Lipumba na Sakaya hawakupata nafasi
ya kujitetea kutokana na kutohudhuria mkutano huo wakati Shashi alipata nafasi
ya kujitetea kutokana na uwepo wake lakini utetezi wake haukuzaa matunda.
Katiba ya chama hicho haiwapi nafasi wabunge hao kukata rufaa kutokana na
uamuzi wa Baraza hilo.
Uamuzi huo umekuja ikiwa ni siku
chacha baada ya Mkutano Mkuu Maalum wa Chama hicho uliolenga kumchagua
Mwenyekiti Mpya kuvunjika kutokana na kuwepo vurugu kubwa baada ya Profesa
Lipumba kuingia ndani ya ukumbi huo na wafuasi wake wakitaka barua yake ya
kutaka kurejea kwenye nafasi yake ijadiliwe na kukubaliwa.
Hata hivyo, kura zilizopigwa na
wajumbe wote zaidi ya 800, ni kura 14 pekee zilizotaka Profesa Lipumba aendelee
na nafasi ya uenyekiti.

No comments:
Post a Comment