
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa ameandika barua
kuhusu operesheni ya chama chake iliyopewa jina la Ukuta na jinsi ambavyo jeshi
la Polisi na Serikali lilivyopanga ‘kuubomoa’.
Katika waraka huo, Lowassa ameeleza kuwa ameamua kushika kalamu
na kuandika masikitiko yake kuhusu hali ya amani nchini akidai Serikali imekata
mkono wa amani.
Ameeleza kuwa Serikali imekandamiza upinzani na demokrasia na
ndio chanzo cha wao kuanzisha UKUTA kupinga ukandamizaji huo.
“Binafsi nafurahishwa na kutiwa moyo na jinsi watanzania
walivyoipokea Operesheni hii, pamoja na vitisho vya dola,” ameandika. “Siku
zote sisi Chadema na Ukawa kwa ujumla ni wenye kulitakia amani na utulivu Taifa
letu. Maandamano haya ya Septemba 1 ni ya amani, lakini vitendo vya jeshi la
polisi vimewapa wasiwasi Watanzania,” Lowassa ameongeza.
Katika andiko hilo, Lowassa amedai kuwa amekuwa akipigiwa simu
na viongozi wastaafu pamoja na watu mashuhuri wakimshauri kushawishi wakae na
Serikali kuzungumza ili kuepusha taifa kujiingiza katika machafuko. Aliongeza
kuwa kukutana na Rais John Magufuli katika Jubilee ya miaka 50 ya ndoa ya Rais
Mstaafu, Benjamini Mkapa ni sehemu ya juhudi hizo.
“Nyote ni mashahidi wa tukio la kukutana na Rais Magufuli katika
Jubilei ya miaka 50 ya ndoa ya mzee Mkapa. Ulikuwa ni mwanzo wa juhudi zetu za
kuwanyooshea mkono wa amani. Lakini tunashangazwa wenzetu hawako tayari
kuupokea mkono huo,” ameandika.
Aliongeza kuwa katika kikao cha juzi cha ndani cha chama hicho
kilichofanyika katika Hotel ya Giraffe jijini Dar es Salaam walipanga
kuzungumzia jinsi ya kuunyosha zaidi mkono wa amani lakini Jeshi la Polisi
‘liliukata’.
“Kitendo kile kwangu binafsi kimezidi kuniimarisha na kunipa
nguvu zaidi ya kudai demokrasia na kuheshimu katiba ambayo viongozi wetu
waliapa kuifuata na kuitetea,” unasomeka waraka wa Waziri Mkuu wa zamani, Lowassa.


No comments:
Post a Comment