Sheria ya Fedha ya Mwaka 2016
iliyopitishwa kuhusu utozaji ushuru kwenye ada ya kutuma na kupokea fedha
kwenye miamala ya benki na simu, imeanza kuzaa matunda kutokana na ongezeko la
mapato lililoanza kushuhudiwa kutoka kampuni za simu.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Miundombinu iliyokutana jana na Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), iliambiwa
kutokana na sheria hiyo iliyopitishwa Bunge baada ya kupitisha bajeti ya mwaka
huu, mwezi uliopita serikali imeshuhudia ongezeko kubwa la mapato, yaliyotolewa
na kampuni za simu.
Taarifa hiyo ilitolewa jana kwenye
Kamati ya Kudumu ya Miundombinu, imeonesha Kampuni ya Vodacom ilikuwa ikitoa
kodi ya ushuru wa bidhaa kwa fedha zinazotumwa kwa wastani wa Sh milioni 360
kwa mwezi, lakini baada ya mabadiliko ya sheria, Julai pekee mwaka huu imelipa
Sh bilioni 1.9.
Mwakilishi wa Kamishna Mkuu wa
Mamlaka ya Mapato (TRA), Godwin Barongo aliiambia kamati hiyo kuwa kwa upande
wa Kampuni ya Tigo, walikuwa wanatoa wastani wa Sh milioni 250 kwa mwezi,
lakini sasa wametoa Sh bilioni 1.48.
Barongo ambaye ni Meneja Msaidizi,
Kitengo cha Walipa Kodi Wakubwa TRA alikuwa akizungumzia namna Mtambo Maalumu
wa Kusimamia Mawasiliano na Udhibiti wa Mapato yatokanayo na Simu (TTMS)
unaosimamiwa na Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) ulivyowezesha kufanikisha
ukusanyaji mapato.
“Pamoja na mabadiliko ya sheria
yaliyoanza mwezi Julai mwaka huu, kampuni za simu zilikuwa zikitoza transfer,
lakini sheria ilikuwa haigusi kwenye kutoa, Baada ya hiyo, tuligundua kuwa sasa
kamisheni nyingi zilipelekwa kwenye kutoa kwa sababu hakuna tozo na kwenye
transfer zinapungua,” alisema Barongo.
Aliendelea kusema, “Kwa
hiyo mabadiliko haya ya sheria ya sasa hivi ambayo tunatoza kwenye kuweka na
kutoa, yametusaidia.”
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso alisisitiza kuwa wabunge
wanategemea Wizara ya Miundombinu kupitia sekta ya mawasiliano, ichangie mapato
mengi kwa serikali.
Baada ya Bunge kupitisha mabadiliko
ya sheria ya fedha yaliyopitisha utozaji kodi ya ushuru wa bidhaa katika
miamala ya benki na simu za mkononi, ulijitokeza mjadala ambao baadhi ya watu
walidai ushuru huo utaathiri wateja wa kampuni za simu na benki.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk
Philip Mpango alifafanua kwamba serikali imeamua kutoza ushuru kwenye ada ya
kutuma na kupokea fedha au vyote kwa kadri itakavyotozwa akisisitiza kwamba
utalipwa na benki na kampuni na si mtumiaji au mpokeaji wa fedha katika miamala
itakayofanyika.

No comments:
Post a Comment