
WANANCHI wametakiwa kutumia tafiti
zilizopo ili kuboresha kilimo kuwa cha kisasa na chenye tija ili kiweze
kuwakwamua na umaskini.
Ushauri huo ulitolewa na Waziri
Mkuu mstaafu, Edward Lowassa baada ya kutembelea mabanda kwenye uwanja wa
maonyesho ya kilimo wa Mwalimu J. K. Nyerere mjini Morogoro juzi.
Lowassa alieleza kuvutiwa na
mafanikio makubwa na ubunifu kwenye sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi na kutoa
wito kwa wananchi kujitokeza zaidi katika maonyesho hayo siku za usoni kwa
kujifunza.
Aidha, Lowassa aliwashauri vijana
kutumia maonyesho kama hayo kuwasilisha tafiti walizozifanya katika sekta za
kilimo, mifugo na uvuvi, ili Watanzania wengi waweze kuzitumia kwa manufaa
ikiwamo kujifunza na kubadilisha utendaji wa mazoea na kuwa wa kisasa kwa faida
yao na taifa.
Lowassa alisema maendeleo duniani
yanafikiwa kutokana na tafiti na kushauri kama Watanzania watatumia vyema
matokeo ya tafiti zinazoendelea kufanywa na wataalamu, wataweza kufika mbali.
Katika ziara hiyo Lowassa alivutiwa
na banda la Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambamo alipongeza shughuli za
uzalishaji wa kisasa wa mazao mbalimbali ikiwamo mboga.
JKT ilikuwa ikionyesha kilimo cha
kutumia nyumba ya kijani (green house), ufugaji wa kisasa wa mbuzi wa maziwa,
kuku, uvuvi na teknolojia nyingine zinazohusu sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.
Maonyesho hayo ambayo kitaifa
yalikuwa mkoani Lindi, yalifikia kilele jana kwa kuhutubiwa na Makamu wa Rais,
Samia Suluhu Hassan.

No comments:
Post a Comment