
Serikali kupitia Wizara ya Habari
Utamaduni Sanaa na Michezo imedhamiria kurasimisha kazi ya sanaa kuwa shughuli
rasmi ya kiuchumi katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Rais Dkt.John
Pombe Magufuli.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari
Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye alipokuwa akizundua msimu wa
tatu wa kipindi cha televisheni cha kusaka vipaji vya wasanii chipukizi cha
Club Raha Leo Show na kuahidi kutoa ushirikiano kwa wadau wa sanaa na wasanii
ili kufanikisha azma ya serikali ya kurasimisha sekta hiyo kuwa rasmi kama
shughuli ya kiuchumi.
“Tutashirikiana na nyinyi katika
kuiendeleza sekta ya sanaa nchini ili kuwezesha vijana wengi wenye vipaji
kuweza kujiajiri na kuajiri wengine kupitia kazi zao za sanaa” alisema
Mhe. Nape.
Mhe. Nape Moses Nnauye amewaomba
wadau mbalimbali kujitokeza kudhamini mashindano mbalimbali ya kuibua vipaji
vya wasanii chipukizi ili kuweza kufikia malengo ya kuendeleza sekta ya sanaa
nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Dkt Ayoub Rioba amesema kuwa Shirika la
Utangazaji Tanzania (TBC) litaendelea kushirikiana na wadau wa sanaa nchini
kuibua na kuendeleza vipaji vya wasanii mbalimbali ili kuwezesha sanaa kuwa
ajira rasmi katika kuinua kipato cha msanii na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Naye Mratibu wa Club Raha Leo Show
Bibi. Susan Mungi amesisitiza wasanii kuheshimu kazi zao na kuzifanya kwa
ustadi mkubwa kwani ndio nyezo muhimu katika kuendeleza kazi ya sanaa nchini kwa
kuifanya kuwa kazi mojawapo ya kiuchumi.
Club Raha Leo Show ilianzishwa kama
Kipindi cha redio kilichorushwa Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) na baadae
kuwa shindano kubwa Tanzania la kusaka, kuibua na kuendeleza vipaji vya wasanii
wanaochipukia nchini, na huu ni msimu wa tatu wa shindano hilo.

No comments:
Post a Comment