SERIKALI kupitia Ofisi ya Mwendesha
Mashitaka (DPP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, imetakiwa kufanya utafiti wa
kina katika mashauri inayoyafungua mahakamani.
Kauli hiyo ilitolewa mjini Arusha jana
na Wakili wa Kujitegemea, Charles Abraham, aliyekuwa akiwawakilisha watuhumiwa
29 katika kesi iliyofunguliwa na Jamhuri dhidi ya Mbunge wa Arumeru Mashariki,
Joshua Nassari (Chadema) na madiwani 28 wa chama hicho wakituhumiwa kuvunja
uzio wa thamani ya Sh milioni saba.
Akizungumza nje ya viwanja vya
Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha baada ya Hakimu Mkazi, Desder Kamugisha kuifuta
kesi hiyo, Wakili Abraham alisema uamuzi huo ulitolewa baada ya Serikali kukosa
ushahidi.
“Ni rai yangu kwa Serikali
kwamba iwe inafanya utafiti katika mashauri inayoletewa kabla haijapeleka kesi
mahakamani. Hii itasaidia kuondoa gharama zisizo za lazima na usumbufu kwa watu
na jamii wakiwamo viongozi,” alisema Wakili Abraham.
Awali, mahakamani hapo, upande wa
Jamhuri ukiongozwa na Wakili Blandina Msawa, uliwasilisha ombi la kutokuwa na
nia ya kuendelea na shauri hilo, hivyo ulimuomba hakimu huyo kuiondoa
hoja ambayo ilikubaliwa na upande wa utetezi.
Akitoa uamuzi wa kuifuta kesi hiyo,
Hakimu Kamugisha alisema kwa vile upande wa mashitaka umeamua kuiondoa kesi
hiyo, mahakama haitakuwa na kipingamizi.
Mbunge Nassari akizungumzia kufutwa
kwa kesi hiyo, alisema ilifunguliwa kisiasa badala ya kuangalia maslahi ya mali
za Serikali.
Naye Mwenyekiti mstaafu wa CCM,
Yona Nnko ambaye mwaka jana alihamia Chadema, alimpongeza Nassari na madiwani
kwa kufanikiwa kupigania haki ya wananchi wa Arumeru Mashariki.
Nassari na madiwani hao
walifunguliwa kesi hiyo na Jamhuri wakidaiwa kuharibu mali ya Itandumi Makere
katika eneo la Usa River.
No comments:
Post a Comment