
MATABIBU wanne wa Tiba Asilia na
Mbadala akiwemo mmiliki wa Kliniki ya Sure Herbal, Simon Rusigwa wamewasilisha
maombi ya kuomba ruhusa ya kufungua kesi ya kupinga uamuzi wa kufutiwa leseni
za kutoa huduma za kitabibu.
Wamewasilisha maombi hayo katika
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, dhidi ya Baraza la Tiba Asilia
na Mbadala, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Mbali na Rusigwa, matabibu wengine
waliowasilisha maombi hayo kupitia kwa Wakili Dk Lucas Kamanija, ni Abdallah
Mandai wa kliniki ya Mandai Herbalist, Fadhili Kabujanja wa Fadhaget Sanitarium
na John Lupimo wa Lupimo Sanitarium.
Maombi hayo yalitakiwa kusikilizwa
jana mbele ya Jaji Ama–Isario Munisi wa mahakama hiyo, hata hivyo kabla ya
kuanza kusikilizwa, Serikali iliwasilisha pingamizi la awali ikidai kuwa maombi
hayo hayakufuata misingi ya kisheria.
Katika pingamizi hilo serikali
inadai kuwa maombi hayo yana kasoro kwa kuwa waombaji hawajapita njia zote
zinazotakiwa wazifuate ndipo waende mahakamani pia wanadai maombi hayana miguu
ya kusimamia kwa kuwa hati ya viapo vya walalamikaji vina upungufu ya kisheria.
Baada ya kuwasilishwa kwa
pingamizi, Jaji Munisi aliahirisha shauri hilo hadi kesho saa 8 mchana, ambapo
alizitaka pande zote zinazohusika ziwepo ili kusikiliza pingamizi hilo.
Katika maombi yao, matatibu hao
wanadai, wameamua kupeleka maombi hayo mahakamani, kwa kuwa wanaamini
walifutiwa leseni bila kufuata taratibu za kisheria.
Wamedai wanaamini uamuzi
uliochukuliwa umetolewa bila kupitia Kamati ya Maadili ya Baraza la Tiba Asilia
na Mbadala, huku wakidai kuwa huo si uamuzi bali zilikuwa tuhuma mpya, lakini
hawakupewa nafasi ya kusikilizwa.

No comments:
Post a Comment