
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ametoa
siku 14 kwa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Mifupa (MOI) kuangalia matatizo
yaliyopo na kuyafanyia tathmini, huku akisisitiza kambi za upasuaji zirejee na
zianze kazi mara moja ifikapo Agosti 13, mwaka huu.
Alisema bodi hiyo itakapokaa na
kurudisha majibu kwake atafanya maamuzi likiwamo suala la uteuzi wa mkurugenzi
wa taasisi hiyo, akisema imekaimiwa kwa kipindi kirefu na sasa ni wakati wa
kumpata wa kuishikilia.
“Kitu
kinachonisumbua kichwa kwa sasa ni kuhusiana na kambi za upasuaji, naomba
zianze kazi mara moja, wanaoteseka ni wananchi wa hali ya chini maana baada ya
kufutwa kambi za upasuaji ikaanzishwa kambi ya upasuaji wa watu wanaolipia,
wasiojiweza wanahudumiwa vipi?” alihoji.
Kauli ya Ummy imekuja baada ya
kikao cha ndani alichokifanya jana na wafanyakazi wa taasisi hiyo, ambao
walitoa malalamiko mbalimbali kuhusu utendaji wa taasisi, stahiki zao pamoja na
malalamiko mengine waliyoyaandika kwenye makaratasi na kuwasilisha kwake.
“Baada ya
kuwaambia muandike kwenye vikaratasi, nimegundua kwamba mlishindwa kusema wazi
ila molari ya wafanyakazi ipo chini na baada ya kusoma kwa makini nimegundua
hakuna ushirikiano wa kutosha,” alisema Ummy.
Ummy alisema katika kutatua
changamoto kadhaa ndani ya taasisi ataanza kwa kupeleka CT Scan mpya, lakini
pia bajeti ya vifaa tiba kiasi cha Sh3 bilioni.
Aliunga mkono wazo la madaktari wa
taasisi hiyo ambao walimtaka kupeleka muswada bungeni wa kupitisha sheria ya
malipo ya kuchangia huduma katika mfuko wa Trauma Fund kwa watu wote wanaotumia
vyombo vya usafiri ili kuokoa maisha ya wagonjwa wanaopata ajali.
“Naunga mkono
hoja hii, lakini siwezi kuisemea moja kwa moja mpaka ipate baraka kutoka Baraza
la Mawaziri, maana ninachokitaka ni kusaidia maskini wasiojiweza ambao ndiyo
hao kila siku wanagongwa na pikipiki na magari, ndiyo wahanga wa hizi ajali,” alisema Ummy.
Akizungumza kwa msisitizo, Ummy
alisema lengo lake kubwa ni kuhakikisha sekta ya afya inakuwa bora kwa kipindi
chake atakachokuwa waziri wa afya huku akiahidi kushughulikia kero mbalimbali
za wafanyakazi walizoziwasilisha kwake.
Akizungumza awali Kaimu Mkurugenzi
wa Taasisi ya Mifupa (MOI) Dk Othman Kiloloma alisema wanakabiliwa na
changamoto nyingi ikiwemo motisha na posho kwa wafanyakazi.
Alisema deni la MOI limekuwa sababu
ya Taasisi kukosa vifaa na vitendanishi kwa wakati kutokana na wasambazaji
wengi kushindwa kuhudumia.
Dk Kiloloma alisema mwaka 2014
wakati anapokea Taasisi hiyo kama Kaimu Mkurugenzi alikutana na deni kubwa la
stahiki za wafanyakazi kiasi cha Sh4 bilioni pamoja na deni upande wa Saccos
kiasi cha Sh500 milioni na kwa sasa wamefanikiwa kulipia Sh600 milioni.
Alisema jengo jipya la MOI bado
linahitaji kiasi cha Sh20.6 bilioni ili kukamilisha vifaa vinavyohitajika
ikiwemo samani muhimu.
“Tatizo kubwa
tunalopambana nalo hivi sasa ni jengo jipya la MOI, ambalo bado hatujakabidhiwa
mpaka sasa, kwanza lina upungufu mkubwa ikiwemo lifti kutokufanya kazi, jengo
zima ili likamilike linahitaji kiasi cha Sh8.6 bilioni,”alisema Dk
Kiloloma.
Wafanyakazi
wafunguka
Wakitoa malalamiko yao kwa Waziri,
wafanyakazi hao walizungumzia mambo makubwa manne likiwemo la stahiki ya
mishahara yao na malipo, uchakavu wa vifaa tiba, maendeleo ya rasilimali watu
na mrundikano wa wagonjwa.
Pamoja na mambo mengine wafanyakazi
hao walilalamikia suala la kutopandishwa vyeo, kutopanda kwa mishahara na
malipo ya ziada kuwa hayatoshelezi, huku wengine wakifanya kazi kwa miezi sita
bila malipo.
Mmoja wa wauguzi wa MOI, Mwajabu
Ali alisema vitanda vilivyopelekwa na Rais John Magufuli baada ya kuzuiwa kwa
mchapalo, vimekuwa na upungufu mkubwa ikiwemo kukosa matairi, jambo ambalo
linaleta ugumu wa utoaji wa huduma.
Alisema jengo hilo jipya limekuwa
na matatizo ya lifti, hivyo inakuwa kazi kubwa kumsafirisha mgonjwa kutoka
wodini mpaka kumfikisha katika chumba cha upasuaji au kipimo.
“Tunafanya kazi
katika mazingira magumu, vitanda havina matairi, lifti mbovu, hakuna maji,
oksijeni za ukutani hakuna, tunatumia mitungi ambayo hata hivyo ni mizito sana
kuibeba,”alisema Mwajuma.
Mtaalamu wa usingizi ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Chama cha Wauguzi MOI, Lucas Magwisa alisema wauguzi wanafanya
kazi katika mazingira magumu kutokana na stahiki zao kuwa tofauti na madaktari
ambao hata hivyo kazi nyingi wanazifanya wao.

Kaimu Mkurugenizi wa MOI Dkt. Othman Kiloloma akizungumza mbele ya
watumishi wa Taasisi ya mifupa muhimbili (MOI) hawapo pichani kabla ya
kumkaribisha Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Mhe.
Ummy Mwalimu hayupo pichani wakati alipokwenda kusikiliza changamoto za
watumishi hao jijini Dar es salaam.




No comments:
Post a Comment