Watu watatu wanashikiliwa na Jeshi
la Polisi Wilayani Ilemela kwa tuhuma za kujiunganishia umeme kinyemela kwenye
nyumba zao kinyume na utaratibu uliowekwa na TANESCO.
Taarifa ya jeshi la polisi mkoa wa
Mwanza imesema kuwa mnamo tarehe 31.07.2016 majira ya saa 5:10 asubuhi katika
maeneo ya Ilemela Mlimani wilaya ya Ilemela jiji na mkoa wa Mwanza, watu watatu
wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kujiunganishia umeme kinyemela
kwenye nyumba zao kinyume na sheria na utaratibu uliowekwa na TANESCO.
Imewataja watu hao kuwa ni
Boniphace Masamaki miaka 47, Lina Cosmas miaka 26 na Ali Mohamed miaka 30 wote
wakazi wa mtaa wa Ilemela Mlimani.
Aidha watuhumiwa hao waliweza
kukamatwa baada ya kupatikana kwa taarifa kutoka kwa raia wema, ndipo jeshi la
polisi kwa kushirikiana na maofisa wa TANESCO waliweza kufanya msako maeneo
hayo na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao.
Watuhumiwa wote wapo katika
mahojiano na jeshi la polisi wakishirikiana na TANESCO, pindi uchunguzi
ukikamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.
Msako wa kuwasaka watu wengine
ambao wamejiunganishia umeme kinyume na utaratibu bado unaendelea.
Kamanda Wa Polisi Mkoa Wa Mwanza
Naibu Kamishina Wa Polisi Ahmed Msangi anatoa wito kwa wakazi wa jiji na mkoa
wa Mwanza akiwataka kuacha tabia ya kujiwekea umeme kinyemela katika nyumba zao
kwani ni kosa la jinai lakini pia wanahatarisha maisha ya familia pamoja na
mali zao.
Amesema jeshi la polisi kwa
kushirikiana na wananchi wema na maofisa wa TANESCO litahakikisha linawasaka na
kuwatia nguvuni watu wote wanaodaiwa kujiwekea umeme kinyemela kwenye nyumba
zao na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
No comments:
Post a Comment