Mwenyekiti wa Mtaa wa Sangabuye,
kata ya Igombe wilayani Ilemela mkoani Mwanza anayejulikana kwa jina la John
Mayala anashikiliwa na polisi kwa kosa la kumtorosha na kumpa ujauzito
mwanafunzi.
Mwanafunzi huyo amefahamika kwa
jina la Lucy Daudi, anayesoma kidato cha pili katika Shule ya Sekondari
Sangabuye ambaye anakadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 14 hadi 17.
Aidha jeshi la polisi pia
linamshikilia mama mzazi wa mwanafunzi huyo aitwaye Agnes Kadilana mwenye umri
wa miaka 48 mkulima, mkazi wa Sangabuye kwa kosa la kushindwa kutoa ushirikiano
kwa polisi pindi alipohojiwa kuhusiana na tukio hilo.
Inadaiwa kuwa mama huyo alishiriki
katika kumtorosha binti yake kwenda kuishi kinyumba na mtuhumiwa baada ya
kupewa fedha.
Mama huyo amedai kuwa binti yake
aliamua mwenyewe kuacha shule kwa madai kuwa shule imemshinda. "Yeye
mwenyewe alisema hawezi kusoma, akasema ajifunze cherehani, sasa sijui"
Amesema mama huyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza
DCP Ahmed Msangi ametoa wito kwa wakazi wa mkoa huo hususani wanaume wenye
tabia ya kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi pamoja na wasichana wenye
umri chini ya miaka 18 kuacha mara moja kwani ni kinyume cha sheria bila kujali
kama palikuwa na makubaliano au la.
No comments:
Post a Comment