Mwanafunzi wa mwaka wa kwanza,
Kitivo cha Sayansi ya Jamii katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Fredrick
Joseph (25), ameuawa kwa kushambuliwa kwa kipigo na watu wanaosadikiwa kuwa ni
wanafunzi wenzake wakati akitoka klabu ya pombe (Bar).
Tukio hilo lilitokea usiku wa
kuamkia jana katika eneo la chuo hicho ambapo mwanafunzi huyo alisikika akipiga
kelele ndipo walinzi wakafika na kumkuta akiwa anagalagala njiani.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, amesema mwanafunzi huyo ambaye
ametokea Musoma mkoani Mara alishambuliwa kwa kupigwa sehemu mbalimbali za
mwili wake na watu wasiofahamika.
Amebainisha mwanafunzi huyo
alikutwa majira ya saa 10 alfajiri katika eneo hilo la chuo hicho huku akisema
kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa marehemu huyo alikuwa na ugomvi na watu
hao katika klabu ya pombe ya Canival Pub iliyopo chuoni hapo.
“Alipoondoka kurudi bwenini akiwa
njiani alishambuliwa na watu hao wasiofahamika na kujeruhiwa sehemu mbalimbali
za mwili wake, kipigo kilichosababisha kifo chake wakati alipokimbizwa kutibiwa
katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma,” alisema Mambosasa
Amesema mwili wa marehemu
umehifadhiwa katika hospitali hiyo kwa uchunguzi zaidi na hadi sasa hakuna mtu
anayeshikiliwa kuhusiana na tukio hilo.
Alipoulizwa kuwa taarifa za
mwanafunzi huyo kushambuliwa na wenzake, Mambosasa alisema kwasababu inadaiwa
haifahamiki upelelezi bado unaendelea.
“Kwa sababu mwenye bar si yupo,
kama kuna ugomvi ambao ulikuwa unaendelea tutajua tu, nimemuelekeza OCD
kufuatilia ni nani waliokuwa wanakunywa kwenye hiyo bar chuoni, ni lazima tu
watakuwa wanachuo ili tuwabaini,”
Kamanda huyo amesema ameelekeza
uchunguzi wa kina ufanyike kama kulikuwa na ugomvi ndio hao hao walienda
kumtegea njiani.
Chanzo cha habari
ambacho hakikutaka kutaja jina lake kwa madai kuwa siyo msemaji
wa polisi kimesema kuwa marehemu Joseph alikuwa anakunywa pombe pamoja na
marafiki zake lakini baada ya kulewa walianza ugomvi ambao hata hivyo
waliamuliwa.
“Baada ya kuamuliwa ule ugomvi wa
awali ndipo wenzake walipokwenda kumsubiria kwa mbele kwenye kichaka ambapo
walimvamia na kumshambulia na kumwacha karibu ya kufa,” kilisema
chanzo hicho.
Kiliongeza kuwa, baada ya kumwacha
hapo na kutoweka ndipo walinzi wa chuo hicho waliokuwa doria walimuokota na
kumfikisha kwenye kituo kidogo cha polisi kilichopo Chimwaga ambapo alikimbizwa
katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma alipofariki wakati akipatiwa
matibabu.
Chanzo hicho kimesema hakuna
mtuhumiwa hata mmoja anayeshikiliwa na polisi kwa kuwa wote waliomshambulia
walitoroka na hawajulikani walipo.
No comments:
Post a Comment