
JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limesema litavifungia vyuo vyote vinavyotoa mafunzo ya udereva nchini bila ya kuwa na sifa.
Kauli hiyo ameitoa Mkuu wa Kikosi
cha Usalama Barabarani nchini, Kamishina wa Polisi (DCP) Mohamed Mpinga wakati
akifungua mkutano wa pili wa Chama cha Shule Binafsi za Udereva Tanzania
(Chashubuta) uliofanyika Dar es Salaam jana.
"Kuanzia sasa Jeshi la Polisi
halitasita kukifungia chuo chochote cha udereva kitakachokosa sifa kwani kwa
kulea shule mbovu tutaendelea kupata ajali na hivyo kuongeza vifo na
majeruhi" alisema Mpinga.
Mpinga alisema kwa mujibu wa sheria
ya shule za udereva sura 163 ya 1965 (R.E 2002) mpaka sasa jeshi la polisi
limesajili shule za udereva 260 ambazo zitategemewa kutoa madereva bora wenye
ueledi wa kutosha kutokana na kuwa chanzo kikubwa cha ajali ni makosa ya
kibinadamu ambayo yanafanywa na madereva.
Alisema jeshi hilo litafanya msako
nchi nzima kuvibaini vyuo ambavyo havina sifa na wamiliki wake kuchukuliwa
hatua na kuwafikisha kwenye mkono wa sheria.
Mwenyekiti wa Chashubuta Taifa,
Robert Mkolla wakati akisoma risala yao mbele ya Mpinga ambaye alikuwa mgeni
rasmi wa mkutano huo, alisema moja ya changamoto waliyonayo ni baadhi ya wadau
wa sekta ya usafiri na usafirishaji kutoona mchango mkubwa unaofanywa na shule
za udereva za watu binafsi wakiamini kuwa vyuo vinavyotoa elimu nzuri ni vile
vya serikali pekee.
Mkolla alimuomba Kamanda Mpinga
uboreshwaji wa mitaala mara kwa mara ili kwenda na mahitaji ya barabara, vyombo
na wakati na shule hizo ziwe zinashirikishwa katika kutoa michango ya
uboreshaji wa mitaala hiyo.

No comments:
Post a Comment