
WAKATI mwigizaji wa kundi la
Orijino Komedi, Emmanuel Mgaya 'Masanja Mkandamizaji' akiendelea kusakwa, Jeshi
la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema unenguaji uliofanywa na
wasanii wa kundi la Orijino Komedi jukwaani wakiwa wamevalia sare za jeshi hilo
ndiyo sababu ya kuwakamata.
Juzi usiku jeshi hilo liliwatia
mbaroni waigizaji wanne wa kundi hilo kwa kosa la kuvaa nguo zinazodhaniwa kuwa
ni za Jeshi la Polisi kinyume cha sheria na taratibu za nchi.
Waliokamatwa Jumanne na kuachiwa
kwa dhamana juzi ni Lucas Lazaro (Joti), Serious David, Alex John na Isaya
Gideon.
Kaimu Kamishna wa Polisi Kanda
Maalum ya Dar es Salaam, Naibu Kamishna Hezron Gyimbi, akizungumza na waandishi
wa habari jijini Dar es Salaam jana, alisema kitendo hicho cha kunengua mauno
kilidhalilisha jeshi hilo na waliwakamata ili kuwahoji na pindi watakapobaini
uhalali wa sare hizo, watawachukulia hatua zaidi za kisheria.
“Waigizaji hawa wa komedi tumewaita
ili kuwahoji kufahamu uhalali wa sare walizokuwa wamezivaa ambazo zinafanana na
za jeshi hili, kinyume cha sheria za nchi.
“Lakini kama mlivyoona mkanda
waliokuwa wamevaa, una tofauti gani na huu niliovaa?” alihoji Naibu Kamishna Gyimbi huku akionyesha mkanda wake.
Alisema jeshi hilo lina miiko na
kanuni zake, na hawaruhusiwi kushiriki shughuli za sherehe na kucheza wakiwa
wamevalia sare hizo.
“Siyo Jeshi la Polisi tu, hata
wengine; Magereza au JWTZ (Jeshi la Wananchi la Tanzania) huruhusiwi kuvaa sare
zao bila kibali maalum labda cha kutaka kuelimisha jamii… lakini hawa hawakuwa
na kibali na walivaa wakiwa kwenye shughuli ya mwenzao,” alisema.
Naibu Kamishna huyo Gyimbi alisema
jeshi hilo linaendelea kumsaka Masanja kwa kuhusika kwenye tukio hilo likiamini
ni mshiriki anayeweza kufahamu walikozipata sare hizo.
Alisema Masanja ambaye hakuvaa sare
hizo wakati wa sherehe hiyo ya mapokezi ya harusi yake, pia alishiriki kwenye
shughuli hiyo, hivyo wanataka kumhoji wakiamini ana ushahidi wa tukio hilo.
"Masanja tunamtafuta kama
mhusika wa shughuli hiyo ambayo waigizaji wenzake walivaa sare zinazodhaniwa
kuwa ni za Jeshi la Polisi kinyume cha sheria na taratibu za nchi,” alisema.
Aliongeza kuwa Masanja anatakiwa
kujisalimisha polisi na watamkamata mahali popote atakapopatikana.
Video za waigizaji hao wakiwa na
nguo zinazodaiwa na Jeshi la Polisi kuwiana na sare zao, zilisambaa kwenye
mitandao ya kijamii zikiwaonyesha wakitoa burudani kwenye harusi ya Masanja.
Masanja alifunga ndoa, Jumapili
iliyopita na waigizaji hao burudani kwenye tafrija ya kupongeza maharusi.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa
Ubungo (Chadema), Saed Kubenea na mwandishi wa gazeti la Mwanahalisi na Mseto,
Josephat Isango jana waliripoti kituoni hapo kwa ajili ya kuitikia wito wa
jeshi hilo.
Agosti 15, Kubenea aliripoti
kituoni hapo na kuhojiwa juu ya makala iliyochapishwa kwenye gazeti la
Mwanahalisi, wiki tatu zilizopita ikielezea hali ya ukiukwaji wa haki za
kibinadamu Zanzibar.
Isango naye aliripoti kituoni hapo
na kuhojiwa kuhusu habari aliyoiandika kwenye gazeti la Mseto lililofungiwa kwa
miezi 36 na serikali wiki iliyopita.
Isango aliandika habari kwenye
gazeti la Mseto la Agosti 4 hadi 10 yenye kichwa cha habari 'Waziri amchafua
JPM'.
Wote wawili walirudi kuendelea na
shughuli zao na Isango alitakiwa kurudi leo, wakati Kubenea hakupangiwa siku ya
kurudi.

No comments:
Post a Comment