
Daudi Felix Ntibenda jana asubuhi
alikuwa na majukumu ya kufungua mikutano miwili na kufanya shughuli nyingine
kwa nafasi yake ya mkuu wa Mkoa wa Arusha, lakini hakuweza kuyatimiza
kikamilifu majukumu hayo kwa kuwa Rais John Magufuli alikuwa na mawazo tofauti
na mipango yake.
Ingawa haikufahamika sababu ya
kuondolewa kwake, huenda mvutano baina yake na Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa
ukawa umechangia.
Saa 2:12 asubuhi jana, Ofisi ya
Waziri Mkuu ilikuwa imeshatoa taarifa kuwa uteuzi wa Ntibenda umetenguliwa na
nafasi yake imechukuliwa na Mrisho Gambo ambaye aliteuliwa hivi karibuni kuwa
mkuu wa Wilaya ya Arusha.
Taarifa hiyo ya Ofisi ya Waziri
Mkuu haikueleza sababu za kutenguliwa uteuzi wa Ntibenda ambaye amekuwa Arusha
tangu mwaka 2014.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo,
Ntibenda, ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Karatu kabla ya kuteuliwa kushika
wadhifa huo mwaka 2014, amehamishiwa ofisi ya Waziri Mkuu ambako atapangiwa
kazi nyingine.
Jana, Ntibenda alikuwa akisubiriwa
kufungua mkutano wa shirika la kimataifa la afya kwa vijana (AMREF) na tayari
tangu asubuhi alikuwa ofisini kwake kujiandaa kwa majukumu hayo ya siku.
Mbali na mkutano huo, Ntibenda
alitarajiwa kushiriki kama mwenyeji katika mkutano wa Mfuko wa Maendeleo
(Tasaf) ambao ulishirikisha wakuu wote wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini pamoja na
wakuu wa wilaya.
Kwenye mkutano wa AMREF, Ntibenda
alisubiriwa kwa muda mrefu hadi habari za kutenguliwa kwa uteuzi wake
ziliposambaa, ndipo akateuliwa mganga mkuu wa mkoa, Frida Mokiti kufungua
mkutano huo.
Habari za uhakika kutoka ofisi ya
mkuu wa mkoa zinasema kuwa kabla ya kuibuka kwa taarifa za kutenguliwa kwake,
Ntibenda alikuwa na mazungumzo na Gambo ofisini kwake.
Haikujulikana mara moja mambo
waliyozungumza wawili hao, ingawa tangu Ntibenda ateuliwe kuwa Mkuu wa Mkoa wa
Arusha kumekuwa na utulivu wa kisiasa.
Ntibenda alikuwa kwenye mzozo na
viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), ambao walikuwa wakimlalamikia
kuingilia majukumu ya jumuiya hiyo.
Mwenyekiti wa UVCCM wa mkoa, Lengai
ole Sabaya aliwaambia waandishi wa habari mapema wiki iliyopita wakati akisoma
maazimo ya kamati ya utekelezaji, kuwa mkuu huyo anakwamisha utendaji wao.
Katika taarifa hiyo UVCCM ilisema
kitendo cha Ntibenda kuingilia kati sakata la mikataba ya wapangaji katika
maduka ya jumuiya hiyo ni kuwakwamisha.
Baadaye kundi la viongozi hao wa
UVCCM pia lilidaiwa kuandika barua ya kumlalamikia Ntibenda kutokana na
kutoridhishwa na utendaji wake.
Hata hivyo, Ntibenda alikanusha
tuhuma zote za UVCCM kumtetea mmoja wa wapangaji na kusema anasikitishwa na
madai hayo dhidi yake.
Uteuzi wa Gambo
Wakati Ntibenda akienguliwa, baadhi
ya viongozi wa UVCCM jana walikuwa wenye furaha baada ya Gambo kupandishwa
cheo.
Mbunge wa viti maalumu, Catherine
Magige alimpongeza Rais Magufuli kwa uteuzi wa Gambo ambaye alisema ni zao la
jumuiya hiyo.
Magige alisema uteuzi huo
unaonyesha jinsi gani Rais Magufuli alivyo na imani na vijana na akawataka
kuendelea kumuunga mkono.
“Tunaamini Gambo ataleta mabadiliko
makubwa ya utendaji katika Mkoa wa Arusha kwa kuwa ni mchapakazi,” alisema.
Wakati Magige akisema hayo, Ole
Sabaya alisema Rais Magufuli amesikia kilio chao.
“UVCCM tulikuwa na malalamiko juu
ya utendaji wa mkuu wa mkoa, sasa tunashukuru sana Rais Magufuli kusikiliza
kilio chetu,” alisema Ole Sabaya.
Kuondolewa Ntibenda
Lakini hali ilikuwa tofauti kwa
mbunge wa Arusha, Godbless Lema aliyesema anaona vurugu zikirudi na kwamba
uteuzi wa Gambo ni kama mkakati wa kuhakikisha wapinzani wanasambaratishwa
mkoani Arusha ambako ni moja ya ngome za Chadema.
Lema, ambaye amekuwa katika mgogoro
na Gambo katika siku za karibuni, alisema kada huyo ameteuliwa ili kuidhibiti
Chadema, jambo ambalo chama hicho hakitakubali.
“Hivi karibuni nilimwambia mkuu wa
mkoa Ntibenda kuna watu wanakutafuta, sasa wamefanikiwa. Lakini mimi naona
Arusha ijayo itakuwa na vurugu tofauti na utulivu uliopo sasa,” alisema.
Hata hivyo, alisema Chadema
imejipanga kuendelea kufanya siasa za kistaarabu na kamwe haitakubali
kuhujumiwa na mtu yeyote yule.
Alipotafutwa jana asubuhi, Gambo
alisema hana cha kuzungumza na kwamba hakuwa na taarifa rasmi.
Gambo, ambaye jana alishiriki
mkutano wa Tasaf kwa nafasi yake ya mkuu wa Wilaya ya Arusha na baadaye
kuondoka, alisema alikuwa hajapata taarifa rasmi.
Hata hivyo, akiwa kwenye mkutano
baadhi ya wakuu wa mkoa na wakuu wa wilaya za mikoa ya Kanda ya Kaskazini,
walimpongeza kwa uteuzi huo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha,
Richard Kwitega alisema alipata taarifa za uteuzi huo jana asubuhi na alipata
maelekezo kuwa Gambo anatakiwa Dar es Salaam.
“Nilipata taarifa rasmi ya uteuzi
wake na tayari tulikuwa naye hapa ofisini ili kuweka taratibu za kwenda
kuapishwa,” alisema.
Alisema Gambo atarejea Jumamosi na
atapokewa na wafanyakazi na baadaye kushiriki mapokezi ya Mwenge wa Uhuru
wilayani Ngorongoro.

No comments:
Post a Comment