
Makamu wa Rais wa Kampuni ya Total
Afrika Mashariki Bw. Javiero Rielo amemhakikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kuwa maandalizi ya kuanza kwa ujenzi wa
bomba la mafuta la kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini
Tanzania yanaendelea vizuri na kwamba kampuni hiyo imedhamiria kuhakikisha
mradi huo unatekelezwa kwa mafanikio.
Bw. Javiero Rielo amesema hayo jana
tarehe 24 Agosti, 2016 Ikulu Jijini Dar es Salaam alipokutana na Rais Magufuli
kwa lengo la kumpa taarifa juu ya maendeleo ya maandalizi ya kuanza kwa ujenzi
wa bomba la mafuta.
Mradi huo utahusisha ujenzi wa
bomba lenye urefu wa kilometa 1,410 ambalo litasafirisha mafuta ghafi kutoka
ziwa Albert nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga nchini Tanzania na unatarajiwa
kuzalisha ajira za moja kwa moja 1,500 na ajira zisizo za moja kwa moja 20,000.
Gharama za mradi wa ujenzi wa bomba
hilo zinatarajiwa kuwa takribani Dola za Kimarekani Bilioni 4 na Kampuni ya
Total inasema fedha hizo zipo tayari.
Akizungumza baada ya kupokea
taarifa hiyo, Rais Magufuli amesema anaamini kuwa mradi huo utakuwa na manufaa
makubwa kwa Tanzania, Uganda, Kampuni ya Total na nchi jirani.
Amebainisha kuwa pamoja na kwamba
Tanzania ipo katika mazingira mazuri ya kutekeleza mradi huo, Serikali yake
itatoa ushirikiano mkubwa ili kufanikisha mradi huo.
Katika hatua nyingine, Rais
Magufuli amepokea hati za utambulisho kutoka kwa mabalozi watatu
wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.
Mabalozi waliowasilisha hati zao ni
Mhe. Ian Myles – Balozi wa Canada hapa nchini, Mhe. Prasittiporn Wetprasit –
Balozi wa Thailand hapa nchini mwenye makazi yake Mjini Nairobi nchini Kenya na
Mhe. Harald Gunther – Balozi wa Austria hapa nchini mwenye makazi yake Mjini
Nairobi nchini Kenya.
Pamoja na kuwasilisha hati zao za
utambulisho Mabalozi hao wameelezea kufurahishwa na mahusiano na ushirikiano
mzuri uliopo kati ya nchi zao na Tanzania na wameahidi kufanya kazi bega kwa
bega na Serikali ya Tanzania ili wananchi wa pande zote wanufaike na matokeo ya
ushirikiano huo hususani katika uwekezaji na biashara.
Kwa upande wake Rais Magufuli
amewahakikishia Mabalozi hao kuwa Serikali yake itaendeleza na kukuza zaidi
ushirikiano kati ya Tanzania na nchi hizo na ametoa wito kwa Mabalozi hao
kuzishawishi zaidi nchi zao na wawekezaji katika nchi hizo kushirikiana na
Tanzania katika ujenzi wa viwanda, uongezaji thamani ya madini, kuendeleza
kilimo hususani kilimo cha umwagiliaji, uzalishaji wa nishati na biashara
mbalimbali.
Pia Rais Magufuli ametoa wito kwa
Mabalozi wa Thailand na Austria kuanzisha ofisi za Ubalozi hapa nchini ili
kurahisisha na kuharakisha shughuli za kibalozi.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano,
IKULU
Dar es Salaam
24 Agosti, 2016

No comments:
Post a Comment