
WIZARA ya Maliasili na Utalii
kupitia Huduma za Misitu Tanzania ( TFS) imepiga marufuku usafirishaji wa mazao
ya misitu ikiwemo mkaaambapo
mfanyabiashara anayefanya biashara hiyo, atapaswa kuwa na vigezo ambavyo
Serikali inavihitaji, tofauti na hapo sheria itachukua mkondo wake.
Imesema zuio hilo linakwenda
sambamba na kupiga marufuku usafirishaji wa magogo ya miti kwenda nje ya nchi,
magari kubeba mbao yakiwa yamefunikwa, pikipiki na baiskeli kubeba mkaa kwenda
sehemu moja hadi nyingine mijini na vijijini.
Akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam juzi, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS),
Profesa Dos Santos Silayo, alisema uamuzi huo ni moja ya mikakati ya kukusanya
maduhuli stahiki ya rasilimali za misitu na kuwabana wakwepa ushuru.
Alisema moja ya majukumu ya TFS, ni
kuhakikisha inaanzisha na kusimamia rasilimali za misitu ili zisaidie ustawi wa
taifa kwa kizazi cha sasa na kijacho, hivyo ni lazima wananchi wafahamu kuwa ni
kosa kuvuna hovyo misitu na bidhaa zake bila kibali.
Mtendaji huyo alisema kila zao
linalotokana na misitu ni lazima lilipiwe ushuru stahiki na kukatiwa risiti,
hivyo kukwepa kufanya hivyo kwa kutumia njia mbalimbali zinazokatazwa ni
kuvunja sheria na kuiibia serikali mapato.
“Mazao ya misitu, ikiwemo mikaa ni
kosa kuuzwa na kusafirishwa bila kuwepo kibali na risiti. Muuza mkaa lazima uwe
na risiti, na wewe mnunuzi tukikukamata na gunia la mkaa na huna risiti
utawajibika.
“Tunataka kuhakikisha maduhuli ya
mazao ya misitu yanakusanywa ili kupata matumizi endelevu ya rasilimali za
misitu hivyo ni biashara hii ya miti, mkaa na mazao ya nyuki inatakiwa iwe
wazi.
“Ni marufuku kusafirisha mazao ya
misitu usiku, kama mtu ana vigezo vyote tunavyovihitaji kusafirisha mazao ya
misitu anatakiwa kusafiri kuanzia saa 12 asubuhi mpaka saa 12 jioni, ikipita
hapo, weka pembeni gari mpaka asubuhi,” alisema.
Aidha alisema TFS chini ya Wizara
ya Maliasili ina Meneja miti kwenye kila wilaya, ambao wanafanya kazi kwa
karibu na Maofisa Watendaji wa vijiji ambao hushirikiana kutoa vibali kwa
kuvuna miti stahiki kisheria na kutoa risiti.
Alisema risiti hizo pamoja na
vigezo vingine ikiwemo kuwa na usajili wa TFS, leseni ya biashara na namba ya
utambulisho wa mfanyabiashara (TIN), hati ya kusafirisha mazao ya misitu
humfanya mfanyabiashara kuruhusiwa kuendelea na biashara ya mazao ya miti nchini.
Profesa Silayo alisema TFS
wataendelea na majukumu yao kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kutekeleza maagizo
yaliyotolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alipozungumza na watumishi wa
wizara hiyo mapema mwezi uliopita.
Baadhi ya maagizo hayo likiwemo la
kupunguza vizuio kwenye maeneo mbalimbali ya nchi, Silayo alisema wanafanya
utafiti kujua kizuizi gani kitolewe na kipi kibaki sambamba na kubana uvunaji
holela wa misitu.
Alisema lengo lao si kukamata
magogo baada ya kuvunwa bali ni kuzuia misitu isiharibiwe hivyo inapotokea,
hutumia vizuio hivyo kukagua na kukamata nyara hizo za serikali ili kuongeza
maduhuli kwa mujibu wa sheria.
“Tumeanza kutekeleza maagizo ya
Waziri Mkuu, ambayo kiuhalisia yana ukweli mkubwa kwa hiyo tunataka kuondoa
vizuizi visivyo na tija lakini pia kuwasisitizia watu wetu kule vituoni
kuzingatia weledi.
“Tayari tumeanza kutumia mashine za
kielektroniki za malipo yaani EFD kwenye vizuio vyetu mikoa ya Dar es Salaam,
Pwani na Morogoro na tutaendelea kuzisambaza maeneo mengine mara tu TRA
watakapoziingizia program yao ya malipo,” alisema.
Alisema wana changamoto kadhaa
ikiwemo uhaba wa vitendea kazi hususan magari lakini wanafanya jitihada
mbalimbali kuhakjikisha wanazitatua ili misitu iwe na mchango kwenye pato la
taifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa
Mipango na Matumizi Endelevu ya Rasilimali Misitu wa TFS, Mohammed Kilongo,
alisema kitakwimu asilimia 94 za kaya zote takriban milioni tisa nchini
zinatumia mkaa kama nishani kuu, huku maeneo ya mijini pekee ikiwa na asilimia
38 za watumia mkaa.
“Mahitaji ya miti ni mita za ujazo
62.3 huku uwezo ukiwa ni mita za ujazo 42.8 hivyo uharibifu wa misitu unafika
hekta 372,000 kwa mwaka sawa na asilimia 1.1 ya eneo lote lenye miti,” alisema Kilongo.
Alisema kwa takwimu hizo, miti na
misitu nchini imekuwa ikipungua kwa kiasi kikubwa na kusababisha uhitaji wa
hekta mpya 185,000 za misitu inayotakiwa kupandwa maeneo mbalimbali ya nchi.
“Upungufu huu ni kichocheo cha
uvunaji haramu na holela ndani ya misitu ya hifadhi, mapori ya akiba na hata
ndani ya hifadhi za taifa hivyo suala la kuilinda ni jukumu letu sote, kila
gunia lazima lilipiwe ushuru,”alisema.
Pia alisema katika jitihada za
kurudisha misitu iliyopotea, upo mkakati wa kitaifa wa kupanda miti ambapo kwa
kila wilaya imepewa jukumu la kupanda miti milioni moja na nusu kwa mwaka chini
ya uangalizi wa Meneja misitu wa wilaya husika.
Wiki kadhaa zilizopita, Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii
jijini Dar es Salaam, alisema nchi inageuka jangwa kutokana na misitu mingi
kukatwa kiholela huku maduhuli ya serikali yakipotea.
Kauli hiyo inaonekana kuanza kuzaa
matunda baada ya TFS kuamua kuongeza kasi ya usimamizi wa rasilimali za misitu
na nyuki nchini kwa siku za hivi karibuni hatua ambayo inadaiwa kuwa endelevu.
TFS inasimamia jumla ya misitu 506
nchini ikiwemo ya asili na kupandwa, pamoja na kusimamia jamii takriban milioni
9.2 za nyuki walioko kwenye misitu hiyo maeneo mbalimbali ya nchi.

No comments:
Post a Comment