
SERIKALI imeanza kuwashughulikia
watumishi walionufaika na fedha za watumishi hewa ambapo hadi sasa watumishi
839 wapo katika hatua mbalimbali wakiwemo waliofikishwa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru) na wengine wanaendelea kuhojiwa polisi kwa ajili
ya kufikishwa mahakamani.
Sambamba na hilo, serikali
inatarajia kutoa ajira mpya 71,496 kwa mwaka huu wa fedha baada ya kukamilisha
uondoaji wa wafanyakazi hewa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Utumishi na Utawala Bora), Angella Kairuki aliyasema hayo wakati akizungumzia
utekelezaji wa mipango na mikakati ya wizara yake katika kipindi cha
‘Tunatekeleza’ kinachorushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1). Kairuki
alisema,
“Kwa sasa tayari wapo watumishi
wameshahojiwa na kuchukuliwa maelezo yao polisi na upelelezi utakapokamilika
watachukuliwa hatua mbalimbali za kisheria, ikiwemo kufikishwa mahakamani…
Tunakamilisha ushahidi na tutawatangazia tutakapokamilisha,” alisema.
Alisema waligundua kwamba kuna
maofisa utumishi na wahasibu ambao siyo waaminifu, badala yake walikuwa
wakielekeza fedha kwa ndugu zao na miradi yao na wengine walishastaafu lakini
bado majina yao yalikuwa yakiendelea kupokea mishahara wakati walitakiwa
kuondolewa kwenye mfumo.
Alisema kwa kipindi cha Machi mosi
hadi Agosti 20 mwaka huu, watumishi hewa waliogundulika ni zaidi ya 16,127 na
kuisababishia serikali hasara ya mabilioni ya fedha. Kwa kipindi cha Agosti
pekee watumishi hao hewa wangelipwa mishahara wangeisababishia serikali hasara
ya zaidi ya Sh bilioni 16.
“Uhakiki huu ni endelevu na
tumegundua changamoto kubwa katika usimamizi wa mishahara ni uadilifu kwa watu
waliokasimiwa madaraka. Maofisa Utumishi, Maofisa Utawala na Wahasibu wamepewa
madaraka lakini wengi wao siyo waaminifu, hivyo kwa sasa tumeweka uwajibikaji
kwa waajiri,” alisema.
Aidha alisema wanaufanyia mfumo wao
maboresho zaidi ili uweze kuchakata taarifa nyingi zaidi ambapo pia sekta ya
mishahara imeshushwa katika ngazi za chini zaidi hasa katika sekta za elimu na
afya ambazo zimekutwa na watumishi hewa wengi zaidi ili waweze kuwa na taarifa
za mtumishi mmoja mmoja.
Alisema upo muongozo ambao fedha za
serikali zinaporejeshwa zinapitia hazina na kusisitiza kwamba wataendelea
kuhakikisha wanasimamia fedha zote ambazo zilichukuliwa serikalini kinyume na
utaratibu na isivyo halali zinarudishwa kwa mfumo sahihi.
Pia alisema wameongeza kasi ili
kuhakikisha kunakuwa na nidhamu ya kazi na uwajibikaji kwa watumishi wa umma, hivyo
wanaanda mkataba wa utendaji kazi kwa watumishi wa umma na ikiwezekana utaanza
kutumika mwaka ujao wa fedha.
Alisema serikali imefanya maboresho
makubwa katika mishahara na motisha kwa ajili ya maslahi ya watumishi wa umma,
sambamba na kuhimiza taasisi mbalimbali kuweka vitendea kazi ili kuwawezesha
wafanyakazi kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Akizungumzia ajira hizo mpya
Kairuki aliwatoa hofu watanzania waliokuwa wanatarajia ajira serikalini na
kusisitiza kwamba walichokuwa wanasubiri ni takwimu halisi kwa taasisi ili
kujua ni watumishi wangapi wameondolewa.
“Baada ya kukamilisha mchakato huo,
hatua nyingine zitaendelea… Hii ni neema kwa waliomaliza vyuo, cha msingi
wavute subira maana tutatoa ajira 71,496 kwa mwaka huu wa fedha na hatukuzifuta
ajira.
"Nawashauri vijana
wasijiingize kwenye makundi yasiyofaa wasubiri ajira zinakuja,” alisema.
Katika hatua nyingine, Kairuki
alisema, wamepokea malalamiko zaidi ya 200 kutokana na ukiukwaji wa sheria ya
maadili ya viongozi wa Utumishi wa Umma ambayo inamnyima mtumishi kutotumia
madaraka yake vibaya.
“Katika malalamiko hayo 142
yanahusu sheria ya maadili. Sekretarieti ya Maadili imefanya uchunguzi wa awali
na malalamiko 12 yataanza kufikishwa Baraza la Maadili na hatua mbalimbali
zinaweza kuchukuliwa ikiwemo kushushwa vyeo au kuachishwa kazi,” alisema.
Pia aliwaagiza maofisa utumishi
kuwahudumia watumishi na kuwapa haki zao ikiwemo kuwapandisha madaraja kwa
wakati pale wanapostahili. Aidha Kairuki alikemea tabia ya baadhi ya watu
kughushi taarifa za utumishi wa umma na kusisitiza kwamba jambo hilo ni kosa
kubwa kwa yeyote anayefanya hivyo.
“Mtu yeyote ambaye anatoa nyaraka
za serikali na siyo mlengwa au anayetoa nyaraka ambayo imewekewa zuio kwa
mujibu wa sheria ni kosa la jinai na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi
yake. Tunawasisitiza watumishi wa umma kuhakikisha wanazingatia sheria hizo na
mwongozo wa utoaji nyaraka na kumbukumbu za taarifa za serikali,” alisema.

No comments:
Post a Comment