
Agosti 22, 2016 Umoja wa Vijana wa
CCM tuliutangazia umma na dunia kwamba ifikapo Agosti 31 mwaka huu tutaitisha
maandamano ya amani nchi nzima yenye lengo la kuunga mkono juhudi za serikali
ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk John Pombe Magufuli kwa utendaji wenye
tija, ufanisi na uliorudisha imani na matumaini kwa wananchi.
Msimamo na dhamira ya kufanya
maandamano hayo ya amani yenye maudhui na kusudio hilo, bado uko pale pale
ingawaje si kwa tarehe tuliopanga na kutangaza awali yaani Agosti 31 mwaka huu.
Jumuiya yetu kama mjuavyo ni ya
Vijana wa CCM, (UVCCM) inapata malezi kwa karibu mno na Jumuiya ya Wazazi ya
CCM. Wiki ya jana Mwenyekiti wa Wazazi Taifa Nd. Abdallah Bulembo alikutana na
waandishi wa habari akitutaka UVCCM tuahirishe maandamano ya Agosti 31 mwaka
huu hadi wakati mwingine.
Kwa mujibu wa Katiba ya Chama Cha
Mapinduzi, Jumuiya ya Wazazi ndiyo Msimamizi wa Malezi, Maadili na Adabu kwa
Vijana wote nchini, sisi UVCCM tunaamini kuwa sikio halishindani na kichwa,
mtoto ni mtoto kwa Wazazi wake hakui, hana jeuri wala ubishi.
Mtoto au watoto wanaokaidi amri,
ushauri au maelekezo ya Wazazi wao huitwa watukutu, wenye viburi, manunda na
wasioambilika. UVCCM si watukutu, hatukufunzwa tuwe wabishi, wakaidi na wenye
viburi. Tumezingatia kutii maelekezo, makatazo na maonyo , tumeambiwa
tuahirishe maandamano yetu nasi tumekubali na kuheshimu mambo tuliyoaswa.
Sambamba na hilo tumepata majibu ya
barua yetu tuliyomwandikia Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP Ernes Mangu)
inayotutaka tuache kufanya maandamano yetu kwa sababu Polisi wamezuia mikutano
ya hadhara ya Vyama vya Siasa na maandamano nchi nzima.
Jambo jingine ambalo limetufanya
pia tuahirishe maandamano yetu ya Amani ni taarifa ya kintelejinsia
iliowasilishwa na Kamati yetu ya Usalama na Maadili ya UVCCM mbele ya kikao cha
Sekreteriet yetu, nayo ilipendekeza suala hilo liahirishwe kwa wakati huu
hadi muda mwingine.
Pia jambo jingine ambalo limefanya
maandamano hayo tuyabatilishe ni kulipisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ
) ambalo litakuwa katika shughuli za maadhimisho miaka 52 tokea kuanzishwa
kwake.
Wanajeshi wetu watakuwa katika kazi
mbalimbali za kijeshi kwenye kambi zao na mitaani kufanya usafi wa mazingira,
hivyo isingependeza na wala si heshima wakati sisi tukiandamana, wao wakifanya
kazi muhimu kila mmoja wetu zinazomgusa badala yake ni vyema kuwaunga mkono
jambo wanalolifanya la usafi wa mazingira.
UVCCM tumekubali, hatutaki kuingia
katika uvunjaji wa sheria hasa baaada ya kutakiwa kuahirisha na mamlaka za
Kisheria hadi wakati mwingine muafaka na si wakati huu.
Tunaelewa kwamba uamuzi wetu wa
awali wa kutaka kuandamana kwa amani hata kama tungenyimwa kibali
ungetugharimu, ungetusababishia madhara na pengine hasara, kwa wakati huu na
kuona jambo lenyewe ni la kuipa Ari serikali katika kuhimiza Uwajibikaji, Utendaji
na Usimamizi bora wa Uendeshaji wa masuala ya kiutawala.
Tulishusha maagizo kwa Makatibu
wetu wote wa Mikoa yote 32 na Wilaya 171 ya Kichama tukiwataka waandike barua
katika Ofisi za Ma RPC na OCD, washirikiane ili kuratibu maandamano na
kuyafanikisha kama tulivyokusudia.
Watendaji wetu wa ngazi husika
wamefuata maelekezo, wametii taratibu zetu za kiutendaji na leo tumewajulisha
tena wasitishe maandamano hadi tutakapowapa tena maelekezo mengine.
Tunawahimiza na kuwataka ni vyema kutii mamlaka za Kikanuni na Kisheria.
UVCCM kwa wakati huu tumeamua
kuachana na maandamano badala yake tunajikita katika matayarisho ya kuwapeleka
Vijana wetu wakashiriki katika Mafunzo ya Siasa, Utawala, Uongozi, Ufundi na
Ujasiriamali yatakayoanza kufanyika katika Chuo chetu kilichopo huko Ihemi
Mkoani Iringa ambapo kitakuwa kielelezo na alama nzuri ya kumuunga mkono
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dk. John Pombe Magufuli kwa vitendo.
Tumewataka Makatibu wetu wa Mikoa
na Wilaya kuendelea na zoezi la Uratibu na Uhakiki kwa Vijana ambao watateuliwa
kushiriki Mafunzo hayo huko Ihemi.
UVCCM tunarejea kusema tena kwamba
dhamira ya maandamano yetu ya kusifu Utendaji wa Serikali ya awamu ya tano iko
pale pale ila tutapanga tarehe nyingine katika wakati ujao badala ya kufanyika
Agosti 31 mwaka huu kama tulivyotangaza hapo awali.
UVCCM tunawataka Vijana wote
kuendelea kuheshimu Tunu ya Amani Umoja na Mshikamo wetu kwa Taifa.
KIDUMU CHAMA CHA
MAPINDUZI
Shaka Hamdu Shaka
(MNEC)
KAIMU KATIBU
MKUU.

No comments:
Post a Comment