Shule za msingi 68 pamoja na shule 22 za sekondari katika wilaya ya
Kinondoni jijini Dar es Salaam, zimebainika kuwa na wanafunzi hewa 5,996. Kati
ya hao, wanafunzi 3,462 ni wanafunzi wa shule za msingi na 2,534 ni wanafunzi
katika shule za sekondari.
Mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Ally Salum Hapi, ameitaja
idadi hiyo jana katika ofisi yake wakati akiongea na waandishi wa habari juu ya
wanafunzi hewa waliopo katika wilaya yake.
“La kwanza tumemwagiza mkurugenzi kuwavua madaraka
walimu wakuu 68 wa shule za msingi ambao watanyanga’nywa vyeo vyao kwa kosa la
udanganyifu wa takwimu juu ya elimu bure,” alisema.
“Lakini la pili tunaandikia
tume ya utumishi wa walimu kupitia kwa mkurugenzi ambaye ndiyo muajiri wao
kuhakikisha kwamba hatua nyingine kali za kisheria zinachukuliwa dhidi ya hawa
walimu wakuu 68 wa wilaya ya Kinondoni, ambao wamedanganya katika taarifa zao
na kuweka idadi ya wanafunzi hewa katika orodha ya wanafunzi wa elimu bure.”
Pia kwa upande wa walimu wakuu wa shule za Sekondari
alisema, ” Walimu wakuu wa shule za sekondari wako chini ya katibu tawala wa
mkoa, tumemuandikia katibu tawala wa mkoa kumuomba awavue vyeo vyao walimu
wakuu 22 wa shule za sekondari zilizopo Kinondoni, ambapo wameleta takwimu za
uongo na wameweka majina hewa ambapo zaidi ya milioni 60 zimekwisha kwenda
kinyume na takwimu halisi katika shule zao.
Alielezea pia hatua zitakazochukuliwa dhidi wakuu hao,
“Kwanza anashushwa cheo atakuwa mwalimu wa kawaida , lakini la pili
atachukuliwa atachukulia hatua nyinginezo za kisheria kwa mujibu wa mamlaka ya
utumishi wa walimu kwa shule za msingi na tatu atalipa fedha zote ambazo
zimepelekwa kule kinyume na utaratibu kwa kutokana na udanganyifu alioufanya.”
“Hatutakuwa na huruma na mwalimu mkuu yeyote
atakayefanya udanganyifu wa takwimu za elimu bure, tutamchukulia hatua kali za
kisheria mwalimu yeyote ambaye ataghushi idadi ya takwimu za elimu bure kinyume
na idadi halisi ya wanafunzi wa elimu bure.”
BY:EMMY MWAIPOPO

No comments:
Post a Comment