
Baada ya kufanya uhakiki wa
Wanafunzi Uongozi wa Mkoa wa Simiyu umebaini uwepo wa wanafunzi hewa 2331
katika shule za Sekondari za Mkoa huo.
Taarifa hiyo imetolewa na Mkuu wa
Mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka wakati alipozungumza na Walimu Wakuu na Waratibu
Elimu Kata mara baada ya kuwakabidhi Vishikwambi (Tablets) vilivyotolewa
na Shirika lisilokuwa la Kiserikali la EQUIP Tanzania kwa ajili ya utunzaji wa
Takwimu muhimu za Sekta ya Elimu,.
Mtaka amesema kati ya Halmashauri
sita za Mkoa huo, Ni Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi tu ambayo haina
wanafunzi hewa wakati Halmashauri ya Wilaya ya Busega ikiwa na wanafunzi
hewa 110, Itilima 2137, Maswa 14, Meatu 125 na Halmashauri ya Mji
wa Bariadi 439.
Kufuatia kuwepo kwa wanafunzi hewa
Mkuu wa Mkoa huo amesema, Serikali Mkoani humo imepanga kufanya mabadiliko ya
Wakuu wa Shule za Sekondari katika Mkoa mzima, wakati taratibu za kinidhamu
zikiendelea kwa wakuu wa shule waliotoa takwimu za uongo za wanafunzi
katika shule zao, wakati kwa upande wa shule za Msingi, mabadiliko yatafanyika
baada ya kumaliza mtihani wa darasa la saba.
Mtaka amesema kabla ya uteuzi wa
wakuu wa shule na walimu wakuu utafanyika upekuzi (vetting) kwa wale
watakaopendekezwa ili kujiridhisha kama wahusika wana sifa na uwezo wa
kuendesha shule na kusimamia fedha za Serikali zinazopelekwa shuleni kwa ajili
ya kugharama elimu ya bila malipo.
“ Serikali inaendelea kupelekea
fedha moja kwa moja katika akaunti za shule, kwa hiyo mkuu wa shule au mwalimu
mkuu ni afisa masuuli katika shule yake. Ipo haja kwa sisi kujiridhisha kama
Serikali kuwa anayeteuliwa kushika nafasi ya kuongoza shule ana uwezo na
sifa ya uadilifu. Sitakuwa tayari kuona katika mkoa huu kuna walimu wakuu
wazoefu wa kula fedha za Serikali na wakaendelea kuongoza shule”alisema Mtaka.
Akitoa shukrani kwa Shirika la
EQUIP Tanzania, Mkuu wa Mkoa amesema Shirika hilo limekuwa msaada katika
kutatua baadhi ya changamoto za Watendaji katika Sekta ya Elimu mkoani Simiyu
ikwa ni pamoja na kuwawezesha Waratibu Elimu Kata kwa kuwapa pikipiki na
kuwapa fedha za mafuta shilingi 206,000 kwa kila mwezi pamoja na kutoa mafunzo
kwa walimu wakuu na walimu wakuu wasaidizi.
Aidha, Mtaka amesema analishukuru
shirika hilo kuona umuhimu wa kutoa vishikwambi kwa Walimu wakuu na Waratibu
Elimu Kata ambavyo ameelekeza vitumike kutunza takwimu sahihi za kieleimu
ikiwemo idadi ya walimu na wanafunzi.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa
wa Simiyu, Jumanne Sagini amewataka Walimu Wakuu na Waratibu Elimu Kata
kuvitunza vishikwambi hivyo na kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa.
Naye Mkuu wa EQUIP Tanzania Mkoa wa
Simiyu, Phoebe Okeyo amesema Vishikwambi hivyo vitawasaidia Viongozi wa
Elimu ngazi ya Mkoa, Wilaya na kata kupata taarifa za masuala mbalimbali
yanayofanyika shuleni.
“Sasa hivi mtegemee kupata taarifa
sahihi katika sekta ya Elimu kwa sababu ya hivi vifaa tulivyovitoa leo,
tumeanza kama pilot study kwa Mikoa ya Simiyu, Shinyanga, Mara, Tabora,
Dodoma,Lindi na Kigoma. Tunatarajia kuongeza mikoa ya Katavi na Singida
Januari, 2017”alisema Okeyo.
Jumla ya Vishikwambi(tablets) 637
vimetolewa kwa Walimu wakuu 516 na Waratibu Elimu Kata 121 kutoka
Halmashauri zote sita za Mkoa wa Simiyu, ambapo kila kimoja kina thamani
ya shilingi 315,000/=.

No comments:
Post a Comment