
Serikali za Tanzania na Israeli
zimekubaliana kuinua Sekta za Maji na Umwagiliaji kwa kuweka mikakati
madhubuti, ili kuleta mapinduzi katika sekta hizo nchini katika kufanikisha
lengo la taifa la kuwa na uchumi wa viwanda.
Makubaliano haya yalifikiwa jana na
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge na Balozi wa Israeli
nchini, Yahel Vilan katika mazungumzo yaliyofanyika katika Makao Makuu ya
Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Ubungo Maji, baada ya Balozi huyo kutembelea
wizara hiyo.
"Tunapenda kushirikiana na
Serikali ya Israeli kwa kupata utaalamu wa kutoa huduma ya majitaka na jinsi ya
kuyatibu na kuyatumia kwa matumizi mengine, ambayo kwa sasa ni moja ya
changamoto kubwa, ikizingatiwa ongezeko la huduma ya majisafi inaambatana na
ongezeko la majitaka na kufikia mwaka 2020 ni lazima tuwe tumefanikiwa katika
jambo hilo", alisema Mhandisi Lwenge.
Waziri Lwenge aliendelea kusema
Tanzania pia ingependa kuwa na ushirikiano na Israeli kwenye kilimo cha
umwagiliaji, lengo ni kuhakikisha Tanzania inaongeza eneo linalotumika kwa
kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 461,326 za sasa mpakakufikia hekta
1,000,000.
Vilevile, kuhifadhi maji kwa
kujenga mabwawa na matumizi ya maji yaliyo chini ya ardhi kwa ajili ya
umwagiliaji kwenye maeneo yenye changamoto ya maji kama Dodoma, Katavi na
Singida ili kuwepo chakula salama na cha kutosha nchini.
Katika mazungumzo hayo Balozi Vilan
alisema maji ni moja ya kipaumbele katika maeneo ya ushirikiano wao na
Tanzania.
Na Israeli iko tayari kuisadia
Tanzania kwenye suala la majitaka, kwani ni taifa linaloongoza duniani kwa
huduma ya kutibu majitaka, zaidi ya asilimia 85 ya majitaka hutibiwa na
kutumika tena kwa matumizi mbalimbali. Hivyo, wako tayari kwa kushirikiana na
Tanzania katika jambo hilo.
"Israel piaipo tayari
kuwajengea uwezo watanzania katika sekta ya kilimo cha umwagiliaji,kwa kwenda
kujifunza Israeli tunavyofanya na jinsi tulivyopiga hatua kubwa katika sekta
hiyo.
"Nina hakika ndani ya miaka
kumi ijayo Tanzania itakuwa imepiga hatua kubwa kimaendeleo katika sekta hii,
kwa kuwa ina maji ya kutosha, ardhi ya kutosha na hali ya hewa ni nzuri kwa
kilimo," alisema Balozi Vilan.
Hii ni sehemu ya ziara ya Balozi wa
Israeli nchini ya kutembelea wizara mbalimbali Tanzania kwa lengo la kukuza
ushirikiano wa nchi hizo mbili katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo.

No comments:
Post a Comment