
Umoja wa Wanawake Viongozi wa Vyama
vya Siasa Tanzania (UWASATA), umepinga maandamano yasiyo na ukomo
yaliyotanganzwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kuwa hayana
tija kwa wananchi na Tifa kwa ujumla.
Akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa umoja huo Cecilia Augustino, alisema
maandamano hayo yanaashiria uvunjifu wa amani ambayo ni urithi wa Taifa la
Tanzania.
Alisema wamefikisha tamko lao kwa
Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi na kumtaka msajili kutoacha
chokochocko hizo ziendelee kwani zitasababisha kutoweka kwa amani nchini.
“Sisi wanawake viongozi wa vyama
vya Siasa Tanzania tunapinga azimio la maandamano yasiyo na kikomo
yanayoandaliwa na chama cha Chadema, hakika maandamano hayo hayana tija kwa
wananchi na Taifa kwa ujumla” alisema Hokororo na kuongeza:
“Mheshimiwa Msajili, chokochocko
hizi zinazofanywa na baadhi ya viongozi wa kisiasa zikiachwa tu bila ya
kukemewa tunaamini tunu yetu ya amani ambayo ni urithi wetu tulioachiwa na
waasisi wetu itatoweka”
Aliongeza kuwa hatma ya maandamano
hayo ni kuingia kwenye machafuko na hatimaye mauaji na mateso kwa wanawake,
watoto na walemavu, mambo ambayo hawatakubali yatokee.
Alibainisha kuwa wanawake viongozi
wa vyama vya siasa wanaamini kuwa siasa ni kushindana kwa hoja na si uvunjifu
wa sheria kwa njia ya maandamano yasiyo na tija kwa wananchi na Taifa.
Aliliomba Baraza la Vyama vya Siasa
kuhakikisha linawajibika katika kulinda demokrasia, amani na ustawi wa jamii
nzima ya Watanzania.
Katika hatua nyingine, umoja huo
unaojumuisha wanawake viongozi wa vyama 22 vya siasa nchini, umeomba kufanya
kongamano la amani lenye lengo la kuhamasisha amani na utulivu nchini.
Hivyo, Hokororo aliwaomba viongozi
wakuu wa nchi kuanzia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais,
Waziri Mkuu, wadau wa amani na mashirika binafsi kushirikiana na umoja huo
kufanikisha kongamano hilo.
“Hakika tunaumia wanasiasa
wanapokuwa chanzo cha migogoro na vurugu kwa Taifa letu.Hivyo tunamuomba Rais
wetu tunajua ni msikivu aweze kuona namna nzuri ya kutafuta suluhu ya
mgogoro huu wa kisiasa” alisema Mwenyekiti Cecilia Hokororo.
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji
Francis Mutungi, tayari ameitisha Baraza la Vyama vya Siasa Agost 30, mwaka huu
ili kutoa fursa kwa pande vyama husika kukaa meza moja na kujadili tofauti
zilizopo na kuzipatia ufumbuzi.
Naye Makamu Mwenyekiti wa umoja huo
Ziada Athumani alisema wanaunga mkono hatua hiyo kwani ndio njia muwafaka ya
pande husika ili kufikia muwafaka kwa njia ya amani.
Katika mkutano huo na waandishi wa
habari, wanawake viongozi wa vyama vya siasa waliwakilishwa na wenzao kutoka
vyama vya Demokrasi Makini, ADA TADEA na Chama cha Umoja wa Demokrasi ya Vyama
Vingi (UMD).

No comments:
Post a Comment