Watu wawili wamekutwa wamefariki
katika nyumba ya wageni ya Kings Rest House iliyopo Mtaa wa Bumila, Gongo la
Mboto jijini Dar huku miili yao ikiwa imeungua moto.
Mmiliki wa gesti hiyo, Damian
Mng’ong’o alisema alifuatwa kanisani jana saa 1.30 asubuhi na kuambiwa kuna
chumba kimoja katika gesti yake kinafuka moshi na aliondoka kanisani kuelekea
ilipo nyumba hiyo.
Alisema alipofika aliona moshi bado
unafuka huku nje kukiwa na umati mkubwa wa watu wakishangaa.
“Tulifanya uamuzi wa kufungua
mlango lakini hatukuona mtu yeyote chumbani, ndipo mmoja wa wafanyakazi
alipofungua mlango wa choo ndani ya chumba tukakuta maiti mbili zikiwa zimechomwa.
"
Alisema mhudumu wa gesti alitueleza
kuwa jana (juzi) saa tano asubuhi alikuja mwanamume mmoja akachukua chumba na
baadaye jioni alikuja kijana mwingine wakawa wameingia wote katika chumba
hicho.
“Baada ya muda nilipiga simu polisi
kuripoti tukio hilo nao waliwasili ndani ya muda mfupi wakafanya uchunguzi wao
na kuhoji baadhi ya watu, baadaye wakawaleta madaktari kupima, kisha wakaondoka
na maiti hizo mbili kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya hatua
nyingine.”
Mfanyakazi wa jikoni katika gesti
hiyo ambaye hakupenda jina lake litajwe alisema watu hao waliofariki ni
wafanyabiashara wanaouza ng’ombe katika mnada wa Pugu na mara nyingi wakija Dar
es Salaam hufikia hapo.
“Wengi wanaofanya biashara ya
ng’ombe wakija hufikia hapa, mpaka sasa sijajua kilichotokea kwa hawa
waliokufa, lakini tukio hili limewashtua wenzao kwani baadhi walipoona tukio
hili wameingiwa na hofu na kuondoka,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala,
Salum Hamduni alisema wanaendelea kuchunguza na taarifa za awali
hazijathibitisha kama waliuawa hapo gesti au sehemu nyingine na kupelekwa
hapo.
“Kuna viashiria kuwa huenda
waliuawa wakaletwa pale kwani wana alama ya kamba katika shingo kama vile kuna
mtu aliwanyonga na katika matumbo yao kuna majeraha kama wamechomwa kitu chenye
ncha kali,” alisema na kuongeza:
“Mpaka sasa uchunguzi unaendelea na
Jeshi la Polisi linafanya kazi yake na tunasubiri taarifa kutoka kwa wataalamu
wa masuala ya uchunguzi na alama za vidole ambayo itaeleza kwa nini wao waungue
lakini nguo zao zisiungue. Pia kitanda na vitu vingine visiungue na kwa nini
watu waende kuzima moto, wakati watu wameshafariki,” alisema
Hamduni.
Hamduni alisema mmoja wa
waliofariki alijiandikisha kama Lameck Ludovick, mfanyabiashara na mkazi wa Dar
es Salaam.
No comments:
Post a Comment