WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema
Serikali haitasita kuwaondoa katika nyadhifa zao Wakurugenzi wote
watakaoshiriki katika kutoa taarifa za uongo kuhusu miradi mbalimbali ya
maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.
“Serikali inatoa fedha kwa ajili ya
kutekeleza miradi ya maendeleo ambapo kuna baadhi ya viongozi wamekuwa
wakiandika taarifa za uongo kuwa mradi umekamilika wakati haujajengwa, hivyo
wakurugenzi watakaoshiriki kutoa taarifa zisizokuwa sahihi wataondolewa,” alisema.
Waziri Mkuu ameyasema hayo jana
jioni (Jumapili, Julai 31, 2016) wakati akipokea taarifa ya mkoa wa Morogoro
mara baada ya kuwasili mkoani hapa kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.
Alisema alitumia fursa hiyo kutoa
wito kwa wakurugenzi katika halmashauri zote nchini kuhakikisha wanatembelea
miradi yote inayojengwa katika maeneo yao ili kufanya ukaguzi na kujiridhisha
kama thamani yake inalingana na kiasi cha fedha kilichotolewa.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu
amesema Serikali aihitaji Halmashauri kutoa ajira za mikataba kwenye kada
zilizopo katika muundo wa ajira hivyo ameziagiza halmashauri zote nchini
kufanya mapitio ya watumishi wa mikataba.
“Tumeruhusu kuajiri kwa mikataba
walimu wa masomo ya sayansi kwa kipindi cha miaka miwili tena kwa waliostaafu.
Kuna kada zilizoko katika muundo wa ajira hizo hatuhitaji watumishi wa mikataba
wakiwemo madereva msiwatumikishe kwa mikataba watakosa stahili zao,” alisema.
Akizungumzia suala la watumishi
hewa mkoani Morogoro Waziri Mkuu alisema ni vema wakaendelea kufanya uchunguzi
na ifikapo mwisho wa mwezi huu wawe wamekamilisha taarifa na kuanza kuchukua
hatua kwa waliohusika kwa waliohusika.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa
Morogoro Dk. Stephen Kebwe katika taarifa yake aliyoiwasilisha kwa Waziri Mkuu
alisema mkoa unaendelea kutekeleza agizo la Rais Dk. John Magufuli la kuzitaka
taasisi zote za Serikali kufanya uhakiki wa mishahara hewa na malipo batili ya
watumishi.
Alisema mkoa umebaini watumishi
hewa 315 ambao wameisababishia Serikali hasara ya sh. bilioni 2.132 ambapo timu
ya uhakiki bado inaendelea na zoezi hilo na taarifa kamili itatolewa mara kazi
hiyo itakapo kamilika.
No comments:
Post a Comment