
Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA) imekamata akaunti za Kampuni ya Sahara Media Group kwa kushindwa kulipa deni la Sh4 bilioni kama kodi iliyopaswa kulipwa na kampuni hiyo.
Taarifa zilizosambaa kupitia
mitandao ya kijamii zimeeleza kuwa akaunti zote za kampuni hiyo zimefungiwa
mpaka pale watakapolipa deni hilo, lakini kampuni hiyo imetoa ufafanuzi.
Ujumbe huo uliongeza kuwa kampuni
hiyo imefikishwa mahakamani na benki moja hapa nchini kwa madai ya kutaka
kulipwa Sh600 milioni, baada ya kuingia makubaliano ya kulipa wafanyakazi wake
mishahara pamoja na mikopo lakini mpaka sasa imeshindwa kurejesha fedha hizo.
Hata hivyo, akizungumzia suala hilo
mwenyekiti mtendaji wa kampuni ya Sahara, Anthony Diallo alikiri mamlaka
hiyo kufungia akaunti ya kampuni yake.
Diallo ambaye ndiye mmiliki wa
kampuni hiyo alisema ni akaunti moja tu iliyofungiwa na kwamba anaamini baada
ya kukutana na kufanya mazungumzo na mamlaka hiyo watafikia muafaka ili
biashara ziendelee kama kawaida.
“Tutalimaliza hakuna kitakachoenda
mrama,” alisisitiza Diallo ambaye aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali
serikalini ikiwamo nafasi ya Waziri wa Maliasili na Utalii na Naibu Waziri wa
Maji, Maendeleo ya Mifugo katika Awamu ya Nne chini ya Rais mstaafu Jakaya
Kikwete.
Amesema deni la TRA linatokana na
kodi iliyopatikana baada ya ukaguzi wa vitabu kwa miaka mitatu.
“Ni ukaguzi wa kawaida hufanyika
kama taratibu. Sasa kwa sababu ya kuhamisha matangazo yetu kutoka analojia
kwenda digitali ilibidi tukope benki, ujenzi na kumaliza mradi imechukua
miaka mitatu. Wakati wote tumekuwa tukilipa riba benki na zinazobaki toka mauzo
ya matangazo tunalipa mishahara, umeme na malipo ya kodi za kawaida,”alisema.
“Ni kawaida ila wamefanya hatua za
kutuaibisha tu. Kampuni yetu ya ving’amuzi ni ya Kitanzania na mapato yote
yanaingia nchini wakati kampuni nyingine kubwa zote ni za kigeni kutoka China,
Afrika Kusini, Mauritius na Kenya! Ukweli sisi tunahitaji kusaidia nchi
kiuchumi na kutuharibia ni hasara kwa nchi.”
No comments:
Post a Comment