
WATU watatu wanaosadikiwa kuwa ni
majambazi wa kutumia silaha, ambao wamehusika kufanya matukio mbalimbali ya
kihalifu katika mkoa wa Dar es Salaam, wameuawa na majambazi wenzao katika eneo
la Vikindu wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.
Licha ya kuuawa kwa majambazi hao,
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limefanikiwa kuwakamatwa watu
zaidi ya saba, wanaosadikiwa kuhusika na tukio la majibizano ya risasi na
polisi, lililotokeo Vikindu lililosababisha kifo cha askari mmoja.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu, Simon Sirro
alisema kabla ya kuuawa watuhumiwa hao walikamatwa katika maeneo tofauti ya
Mbagala, Keko na Kawe jijini humo.
Alisema watu hao walikamatwa kufuatia
tukio la ujambazi, lililotokea Agosti 29, mwaka huu katika Jengo la Sophia
House maeneo ya Veta Changombe, ambapo majambazi hao walidaiwa kupora Sh
milioni 35 na kutoweka kwa kutumia gari aina ya Toyota Noah lenye namba bandia
T 549 BPK.
Aliongeza kuwa uchunguzi wa tukio
hilo, uliendelea kufanyika na Septemba 3, timu ya upelelezi kutoka Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, iliweka mtego na kufanikiwa kuwakamata majambazi hao
watatu na walipohojiwa walikiri kufanya matukio mbalimbali ya ujambazi wa
kutumia silaha na kuweza kutaja silaha mbalimbali walizonazo.
Kamanda Sirro alisema majambazi
hao, waliwapeleka askari eneo la Mbezi Chini katika nyumba waliyokuwa wamekodi
na askari walifanya upekuzi na walifanikiwa kupata silaha mbalimbali, zikiwemo
bunduki 23 na risasi zaidi ya 800 na vitu vinginevyo.
Alitaja silaha hizo kuwa ni bunduki
za kijeshi tatu aina ya SMG zikiwa na magazini nane na risasi 120, bastola 16,
magazini tatu za bastola na risasi moja, Shot gun pump action tatu na risasi
130, bastola 16 magazini na risasi 548 na bunduki tatu aina ya Shot gun na
risasi zake 130.
Aidha alisema walikuta redio za
mawasiliano 12 na chaja zake tatu, darubini za kuonea mbali tatu, pingu za
plastiki 45, majaketi ya kuzuia risasi matatu, mkasi mmoja wa kukatia vyuma,
mtarimbo mmoja, risasi baridi za kutishia 37, boksi moja la kusafishia silaha,
nyundo kubwa moja, pingu za chuma tatu, mashine moja ya kuhifadhia kumbukumbu
na magari mawili.
Alisema uchunguzi wao ulibaini kuwa
majambazi hao Septemba 6, mwaka huu walipora bunduki aina ya Shot gun yenye
namba 006091830, ikiwa na risasi moja katika barabara ya Mbozi Chang’ombe.
Sambamaba na hayo, majambazi hao
walikiri kuhusika na wizi wa mamilioni ya fedha katika Benki ya Habib African
ya Kariakoo mwaka 2014 na Benki ya Stanbic mwaka 2014, wakitumia gari aina ya
Toyota Noah.
Kamanda Sirro alisema baada ya
mahojiano zaidi, majambazi hao walisema wanazo silaha nyingine ambazo
wamezificha Vikindu wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani. Ndipo askari walifuatana
na watuhumiwa hao hadi kwenye msitu wa Vikindu.
Alisema askari walipofika eneo
hilo, walilodai ni karibu na zilipo silaha hizo, walishuka kwenye gari na
kuingia porini wakiwa wamewatanguliza watuhumiwa mbele majira ya usiku.
Aliongeza kuwa wakiwa msituni humo
na askari wakiwa wenye tahadhari kubwa, ghafla walisikia milio ya risasi
ikitokea mbele, ambapo askari walilala chini na baadaye zikisikika sauti
zikisema ‘mmetuua sisi’.
Alisema baada ya risasi za
mfululizo kutulia, askari walishuhudia majambazi hao ambao walichelewa kulala
chini wakati risasi zikipigwa wakiwa wamejeruhiwa sehemu za kifuani na tumboni
huku wakivuja damu nyingi.
Alisema askari walipiga risasi
kuelekeza eneo zilikotokea risasi na walipoendelea kusonga mbele, walikuta
silaha aina ya SMG ikiwa imetelekezwa na haikuwa na risasi ndani ya magazine,
hivyo kufanya idadi ya silaha za SMG kufikia nne.
Aidha alisema askari waliwabeba
majambazi hao na kuwapeleka kwenye gari kuelekea hospitalini, lakini wote
walifariki dunia wakiwa njiani kutokana na kutoka damu nyingi.
Akizungumzia tukio la Vikindu,
Sirro alisema wamefanikiwa kuwakamata watu hao wanaosadikiwa kuhusika na tukio
ambalo lilisababisha kifo cha askari mmoja.
“Majambazi hao walikuwa ni kundi la
kama watu 14 na tayari tumewakamata zaidi ya saba ambao mpaka sasa
tunawashikilia kwa mahojiano zaidi ili kufanikisha upelelezi,” alisema Kamanda
Sirro.
Pia alisema kumekuwa na taarifa
mbalimbali, zikisambazwa katika vyombo vya habari zikidai kuwa katika tukio la
Vikindu, kuna askari anahusika na tukio hilo na kudai taarifa hizo si za kweli
na hakuna askari aliyehusika katika tukio hilo.
Katika tukio lingine, jeshi hilo
limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanne kwa makosa ya wizi wa magari manane,
likiwemo gari moja la kibalozi.
Kamanda Sirro alisema magari hayo
yaliibwa jijini Dar es Salaam na kuuzwa kwa watu mbalimbali jijini hapo na
mikoani na watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa na mara upelelezi
utakapokamilika watapelekwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Sirro alisema katika tukio lingine
jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa sita wanaodaiwa kuhusika na
kuvunja nyumba usiku na kuiba.
Alisema watuhumiwa wote wanaendelea
kuhojiwa na mara upelelezi utakapokamilika watapelekwa mahakamani kujibu tuhuma
zinazowakabili.



No comments:
Post a Comment